Paris Saint-Germain yamweka sokoni Neymar

Thursday September 12 2019

 

LONDON, ENGLAND. MPO? Paris Saint-Germain imeripotiwa kufungua lango Mbrazili Neymar aondoke zake, tena ikiwezekana jambo hilo lifanyike haraka kwenye dirisha la usajili wa Januari litakapofunguliwa.

Tuttosport inaripoti huo ni msimamo wa mkurugenzi wa soka wa mabinga hao wa Ufaransa, Leonardo, akisema mpango wa timu hiyo ni kuachana na Neymar, ambaye ni Mbrazili mwenzake kwenye dirisha la Januari.

Jambo hilo litazileta kwenye vita kali klabu za Barcelona na Real Madrid zilizotajwa kusaka huduma yake kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi. Lakini Juventus nayo inadaiwa kuwamo kwenye mchakamchaka huo wa kusaka huduma ya Neymar.

Sambamba na Neymar, jina jingine kubwa la staa wa soka huko Ulaya, linaloweza kuhama kwenye usajili wa Januari ni la kiungo, Paul Pogba, ambaye anasakwa Real Madrid, Juventus na hata PSG.

Kwa muda mrefu kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi, kiungo Mfaransa, Pogba alikuwa akihusishwa na mpango wa kutimkia Real Madrid.

Neymar alidaiwa kutaka kurudi Barcelona, wakati Pogba ndoto zake kwenda kukipiga Real Madrid.

Advertisement

Uhamisho wa mastaa hao wawili, utatikisa huko Ulaya kwa sababu kuna mastaa kibao watahusika, akiwamo Paulo Dybala, kama Juventus ikiingia ama kumtaka Pogba au Neymar itataka kumweka fowadi huyo Muargentina kuwa sehemu ya dili.

Lakini mastaa wengine wanaoweza kuguswa kwenye usajili huo ni Ousmane Dembele kama Barca itahitaji kumweka kwenye ofa yake ya kumrudisha Neymar huko Nou Camp.

Man United nayo imetangaza wazi Pogba hatauzwa chini ya Pauni 179 milioni, kwenye dirisha hilo la Januari, ikitaka mkwanja huo kurahisha mambo katika kuinasa huduma ya winga matata wa Kingereza, Jadon Sancho, anayekipiga huko Burussia Dortmund.

Barca iko bayana ikimnasa Neymar, basi saini nyingine itakayoisaka ni ya mshambuliaji wa Arsenal, Alexandre Lacazette, huku jambo hilo likielekea kumpa wakati mgumu zaidi Kocha Unai Emery, kwa sababu Man United nayo inaweza kuvamia kwenda kuulizia saini ya Pierre-Emerick Aubameyang kwenda kuziba pengo la Romelu Lukaku, aliyepigwa bei kwenda Inter Milan kwa ada ya Pauni 73 milioni na huko Old Trafford bado hajaletwa straika mwingine.

Advertisement