Nyie chongeni tu, ila Fei Toto amewasikia

Thursday June 27 2019

 

By Khatimu Naheka,Cairo Misri

KIUNGO wa timu ya taifa, Taifa Stars, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amesema anajua kuna mashabiki wanamshambulia sana, lakini amesisitiza anajua watanyamaza tu kwake.

Akizungumza na Mwanaspoti mjini hapa, Fei Toto alisema anajua sababu ya mashabiki kumshambulia ni kutokana na Stars kufanya vibaya dhidi ya Senegal, lakini upepo huo utabadilika.

Kiungo huyo alisema mashabiki wengi hawawezi kuvumilia mara timu inapopoteza, lakini timu ikishinda hubadilika haraka.

“Nawajua mashabiki wa Tanzania wala hawanisumbui kabisa, tena niko sawa kabisa. Muda huu wanaongea hivi kwa vile timu imepoteza tukishinda kila mmoja anakuwa rafiki yako hata yule aliyekuwa anakusema vibaya,” alisema kiungo huyo wa Yanga.

Fei alisema maneno ya mashabiki kamwe haiwezi kumuondoa mchezoni na kwamba tayari ameshajiandaa kukabiliana na hilo na kwamba anajipanga ili kuisaidia timu hiyo katika mechi zilizosalia kama atapewa nafasi na Kocha Emmanuel Amunike.

Katika mchezo huo wa kwanza ambao Stars ilicharazwa mabao 2-0 Fei Toto alionekana kuzidiwa maarifa na viungo wa Simba wa Teranga kiasi cha Kocha Amunike kumpumzisha kabla ya kipindi cha kwanza hakijamalizika kumpisha Faid Mussa ambaye naye alishindwa kufanya lolote.

Advertisement

Katika mechi hiyo, Stars ilitawaliwa katika kila idara na ilishindwa kulenga lango kwa shuti hata moja kati ya matatu pekee waliyopiga kwa dakika zote 90.

Wasenegal walimiliki mpira kwa asilimia 61 dhidi ya 39 za Stars ambayo ilionekana kukosa maarifa ya kwenda sambamba na miamba hao wa Afrika ambao kikosi chao kimejaa nyota wanaocheza soka katika klabu za Ulaya.

Stars leo inashuka uwanjani kuwakabili Kenya katika mechi yao ya pili itakapopigwa kuanzia saa 5:00 usiku kabla ya kumalizana na Algeria Julai Mosi.

Advertisement