Ngassa, Mohamed warejeshwa kikosini Yanga

Thursday August 6 2020

 

By SADDAM SADICK

SIKU chache baada ya uongozi wa Yanga kuachana na baadhi ya nyota wake, wanachama na mashabiki wa chama hilo wameibuka na kupinga kuachwa kwa wachezaji wawili, Mrisho Ngassa na kiraka Jaffary Mohammed wakitaka warudishwe kikosini.

Juzi Yanga ilitangaza kuachana na wachezaji 14 kwa sababu tofauti ikiwamo waliomaliza mikataba na pia walioonyesha kiwango cha chini ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wao wa kuanza msimu ujao wa 2020/21 kwa kishindo.

Katika msimu uliopita wa 2019/2020 Yanga licha ya kumaliza nafasi ya pili, haikuwa na ubora wowote hasa ukilinganisha na watani wao, Simba ambao walifanya vizuri kwa kubeba mataji yote matatu ya Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (ASFC).

Wakizungumza na Mwanaspoti kwa nyakati tofauti, baadhi ya wanachama na mashabiki wa Yanga jijini Mwanza, walisema licha ya mabadiliko waliyoyafanya viongozi yenye lengo la kuleta ushindani, lakini Ngassa na jaffary hawakustahili kuachwa.

Hashim Omary ambaye ni Katibu Mipango wa Yanga Jijini Mwanza, alisema Ngassa alikuwa na mchango mkubwa klabuni, kwani hata mabao aliyokuwa akifunga yalikuwa ya juhudi binafsi akionyesha zaidi mapenzi yake na timu.

“Labda wameangalia ishu ya ufupi wake, lakini sioni sababu ya Ngassa kuachwa au Mohamed, wale jamaa ndio ilikuwa injini ya Yanga, au wametumia vigezo vya urefu na ufupi? Alihoji kiongozi huyo .

Advertisement

Kwa upande wake, Godson Rwegasira alisema bado hajaelewa mantiki ya kuwaacha waondoke kirahisi wachezaji hao, kwani kwa msimu mzima walikuwa na msaada mkubwa hivyo bora viongozi wakae nao meza moja wamalizane.

“Sio sawa kuwaacha.”

Advertisement