Mzimu wa Torres wamtesa Samatta

Monday August 3 2020

 

By ELIYA SOLOMON

KILE ambacho kimetokea kwa nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta akiwa na Aston Villa katika Ligi Kuu England ni kama anateswa na mzimu wa mshambuliaji wa zamani wa Liverpool, Fernando Torres baada ya kutua Chelsea.

Samatta ameonekana kutokuwa kwenye kiwango chake tangu ajiunge na Aston Villa kwa Euro 10.5 milioni tofauti na ilivyokuwa nchini Ubelgiji ambako alikuwa akitesa huku akiwatungua makipa kwenye michezo mbalimbali ya Ligi Kuu nchini humo maarufu kama Jupiler Pro.

Hakuwa tishio kwenye michezo ya Jupiler Pro pekee bali hata kwenye michuano mikubwa barani humo kama vile Ligi ya Mabingwa Ulaya ambayo alicheza msimu uliopita na Europa Ligi alikuwa akitupia tu.

Lakini sasa mambo yamegeuka. Akaunti yake ya mabao akiwa na Aston Villa inasoma bao moja tu alilofunga dhidi ya Bournemouth tangu hapo amejikuta akicheza michezo 13 bila ya kuwa na bao hadi msimu wa 2019/20 unamalizika. Mambo yamekuwa tofauti na vile ilivyokuwa ikitarajiwa.

Kitendo cha kushindwa kuonyesha makali yake tangu ajiunge na Aston Villa katika dirisha la usajili la Januari kimeanza kufananishwa na kile ambacho kilitokea kwa Torres ambaye naye alipotoka Liverpool kwenda Chelsea mwaka 2011 aliandamwa na ukame wa mabao.

Torres alihamia Chelsea wakati wa dirisha la usajili la Januari kama Samatta, akiwa na jezi nambari tisa mgongoni alijikuta akicheza michezo tisa bila ya kucheka na nyavu kitu ambacho kilikuwa hakijazoeleka kwa mshambuliaji huyo wa Kihispaniola.

Advertisement

Aliona mwezi katika mchezo wa 10 msimu huo wa 2010/11 kwa kufunga bao na kutoa asisti moja dhidi ya wagonga nyundo wa London, West Ham Aprili 23, 2011. Wapo ambao waliamini kuwa huo ndio mwanzo wa Torres kuanza kucheka na nyavu lakini haikuwa hivyo na badala yake akamaliza msimu akiwa na bao hilo moja.

Oktoba 2011, wakati Chelsea ikiwa na mchezo wa hatua ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Genk wakati huo Samatta alikuwa TP Mazembe miezi michache akiwa amesajiliwa kutoka Simba, ilibidi David Luiz amfanyie maombi mshambuliaji huyo.

Ukame kwa washambuliaji umekuwa ukipunguza hata uwezo wa kujiamini. Luiz ambaye kwa sasa anaichezea Arsenal, alimfanyia maombi kabla ya mchezo kuanza, Torres akatupia mbili kwenye ushindi wa mabao 5-0 ambao Chelsea iliupata.

Mbali na Torres washambuliaji wengine ambao nao walihama Januari lakini walishindwa kuonyesha makali yao ni pamoja na Philippe Coutinho wakati wa uhamisho wake kutoka Liverpool kwenda FC Barcelona.

Wengine ni Andy Carroll (Newcastle kwenda Liverpool), Wilfried Bony (Swansea kwenda Manchester City), Juan Cuadrado (Fiorentina kwenda Chelsea).

MKURUGENZI MPYA VILLA

Baada ya kushutumiwa kufanya usajili mbovu na kutimuliwa Aston Villa, Jesús García ambaye alikuwa mkurugenzi wa ufundi ndani wa timu hiyo, hatimaye klabu hiyo, imemtangaza Johan Lange kuchukua nafasi yake.

Hii ni mara ya pili kwa Lange kufanya kazi nchini England. Mara yake ya kwanza ilikuwa Julai mosi, 2011 akiwa kama kocha msaidizi wa Wolves kabla ya kupata dili na kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa FC Copenhagen ya Ligi Kuu Denmark.

SIO MCHEZO

Nyota wa Manchester United, Marcus Rashford amekuwa sehemu ya utambulisho wa mpira mpya wa ‘Nike’ ambao utatumika kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu England. Mpira huo unatahamani ya Tsh. 376, 908.

Msimu ujao utakuwa wa pili kwa Mtanzania, Samatta kucheza Ligi hiyo.

Advertisement