Mwantika aomba Azam imuache

Sunday August 02 2020
mwantika pic

BEKI mkongwe wa Azam FC, David Mwantika sasa yupo huru kuanza maisha mapya nje ya matajiri hao wa soka nchini baada ya mkataba wake kubaki miezi mitano.

Mwantika ambaye ameitumikia Azam kwa misimu minane hana mpango kuongeza mkataba ingawa imeelezwa kwamba viongozi walikuwa tayari kumuongeza.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwantika alisema anataka kwenda kutafuta changamoto mpya baada ya kukaa sehemu moja kwa kipindi kirefu. “Ijumaa nimezungumza na viongozi ambapo walionyesha nia ya kutaka kunipa mkataba mpya, lakini nimewaomba waniache ili nikatafute changamoto mpya, mkataba wangu na Azam umebaki miezi mitano.

“Hivyo tumekubaliana kwa nia moja kuwa niwe mchezaji huru kuanzia sasa kuzungumza na timu yoyote na kucheza sehemu yoyote nitakayopata timu, iwe ndani ama nje ya nchi,” alisema Mwantika

Akizungumzia maisha ndani ya Azam, Mwantika alisema: “Nimecheza misimu minane, lakini ndani ya misimu hiyo ni mitano pekee ambayo nimeitumikia na nimecheza soka la uhakika kutokana na mambo mbalimbali yaliyokuwa yanajitokeza juu yangu kwenye timu.”

Mara kadhaa Mwantika alikuwa akikumbana na sakata la kutolewa kwa mkopo na timu yake, lakini alikuwa akigomea mpango huo ambapo msimu huu wakati wa dirisha dogo alitaka apelekwe Lipuli FC ya Iringa ambayo imeshuka daraja.

Advertisement
Advertisement