Simba SC, Yanga zamuibua mafichoni Kichuya

Muktasari:

Kichuya, ambaye kwa sasa anakipiga kule Misri, lakini yuko nchini akijichimbia kule Morogoro, alisema kwa kawaida Simba na Yanga huwa zinatesa kwa zamu huku akisisitiza kuwa wachezaji wanapaswa kufanya kazi yao tu.

Dar es Salaam.Bado homa ya matokeo ya mabao 2-2 katika mechi ya Kariakoo Derby ya Simba na Yanga, imezidi kuwa gumzo kwa mashabiki wa klabu hizo, lakini huku pembeni imemkumbusha mbali winga wa zamani wa Simba, Shiza Kichuya.

Kichuya, ambaye kwa sasa anakipiga kule Misri, lakini yuko nchini akijichimbia kule Morogoro, alisema kwa kawaida Simba na Yanga huwa zinatesa kwa zamu huku akisisitiza kuwa wachezaji wanapaswa kufanya kazi yao tu.

Kichuya, ambaye bao lake la kona iliyokwenda moja kwa moja wavuni bado linakumbukwa hadi sasa katika Derby ya Kariakoo, alisema matokeo hayo yamemkubusha msimu wa 2017/18 ambapo mzunguko wa kwanza Simba ilitangulia kufunga kupitia bao lake kisha Yanga ikachomoa kupitia Obrey Chirwa, jambo ambalo pia liliwaumiza sana mashabiki wao.

Alisema mzunguko wa pili ilikuwa zamu ya mashabiki wa Simba kucheka, ilitangulia Yanga kufunga Simba ikasawazisha na kufunga bao la pili la ushindi.

“Matokeo ya juzi yamenikumbusha mbali, unajua mechi za Simba na Yanga kunakuwa na lawama kila upande unataka ushindi ili mashabiki kutamba mtaani.

“Nimeangalia gemu, kila mchezaji alifanya kazi kwa upande wake na ikumbukwe Simba na Yanga wote walihitaji furaha ya ushindi. Simba ilicheka kipindi cha kwanza, wenzao Yanga wakasaka furaha kipindi cha pili, huo ndio mpira, kikubwa matokeo yote yawe funzo kwa wachezaji,” alisema.

Kichuya ambaye alipata dili la kucheza soka la kulipwa katika klabu ya ENNPI, alisema sare hiyo imeacha funzo katika soka.

Naye Kocha wa zamani wa Yanga, Kenny Mwaisabula alipigilia msumari kwenye kauli ya Kichuya kwamba anayecheka mwisho ndiye anadumu na furaha akimanisha Wanajangwani ndio wenye furaha na sare.

“Anayemalizia kicheko ndiye shujaa ndio maana unakuta mashabiki wa Simba wana hasira hata Yanga ingekuwa hivyo hivyo, wao wangetangulia kufunga na Simba ingezawazisha.”