Minziro aitosa Pamba atimkia Alliance FC

Saturday January 11 2020

Mwanaspoti-Minziro-aitosa-Pamba-Alliance FC-MWANASPORT-Michezo leo-Michezoblog-Habari za Michezo

 

By Saddam Sadick

Mwanza.Klabu ya Pamba imetangaza rasmi kuachana na aliyekuwa Kocha wake Mkuu, Fredy Felix Minziro aliyetimkia Alliance FC ya Ligi Kuu.

Minziro alijiunga na Pamba hivi karibuni akichukua mikoba ya mtangulizi wake, Muhibu Kanu (Boma FC) amesimamia mechi saba ikiwamo moja ya Kombe la Shirikisho na kushinda moja dhidi ya Green Warriors na sare tatu na kupoteza tatu.

Pamba mabingwa wa Kombe la Muungano mwaka 1990 imekusanya pointi 12 na kukaa nafasi ya 10 katika Ligi Daraja la Kwanza katika kundi B.

Mwenyekiti wa kamati ya Mashindano wa Klabu hiyo, Alhaji Majigoro amesema baada ya makubaliano ya pande zote waliafikiana kumruhusu Minziro kusaka maisha mapya.

Amesema kuwa Minziro baada ya kupata ofa hiyo aliwasilisha klabuni na viongozi walijadiliana hadi kufikia uamuzi wa kuachana naye.

"Kuhusu ishu ya Minziro (Kocha Mkuu) kwa sasa siyo kocha wetu tena bali ni mali ya Alliance FC, alipopata ofa alituambia tukajadiliana hadi kumruhusu kwahiyo uongozi unaendelea kuwasiliana na kocha mpya atakayekuja kuendeleza pale alipoishia" amesema Majogoro.

Advertisement

Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Wakili, ameongeza kuwa kwa sasa timu itakuwa chini ya aliyewahi kuwa Kocha na mchezaji wa zamani wa Pamba, Venace Kazungu akisaidiwa na Kocha wa Makipa, Hassan Shehata.

"Kuhusu usajili hadi sasa ni wachezaji watano ambao tumeshakamilisha usajili wao, lakini tutatoa taarifa rasmi Jumanne ya wote tuliosajili na kuacha" amesema Majogoro.

Advertisement