Ancelotti atupiwa virago Napoli ikifuzu kwa 16 bora Ligi ya Mabingwa

Muktasari:

Sababu inayotajwa kuchangia kutimuliwa kwa kocha huyo wa zamani wa AC Milan na Chelsea ni mwenendo mbovu wa klabu hiyo msimu huu katika Ligi ya Serie A.

Naples, Italia. Kocha Carlo Ancelotti amefutwa kazi na Mabosi wa Napoli licha ya kuiongoza klabu hiyo usiku wa jana kutinga katika hatua ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuifunga KRC Genk mabao 4-0.

Mabao matatu ambayo aliyafunga Arkadiusz Milik dhidi ya timu anayoichezea nahodha wa timu ya taifa 'Taifa Stars' Mbwana Samatta huku lingine likifungwa na Dries Mertens, hayakutosha kukinusuru kibarua cha Muitalia huyo.

Napoli ilitoa taarifa za kuachana na Carlo muda mchache baada ya mchezo huo kumalizika kupitia mitandao yao ya kijamii, ikiwemo Twitter, kwa kuandika ujumbe uliosomeka, "Napoli imeamua kuondoa majukumu ya ufundi ya kikosi cha kwanza kutoka kwa Carlo Ancelotti.

"Mahusiano ya urafiki, heshima kati ya Kampuni na rais wake Aurelio De Laurentiis na Carlo Ancelotti vitabaki pale pale."

Sababu inayotajwa kuchangia kutimuliwa kwa kocha huyo wa zamani wa AC Milan na Chelsea ni mwenendo mbovu wa klabu hiyo msimu huu katika Ligi ya Serie A.

Napoli ipo nafasi ya saba katika msimamo wa Serie A huku wakiachwa kwa pointi 17 na vinara wa Ligi hiyo, Inter Milan (38)  ambao wametupwa nje katika Ligi ya Mabingwa Ulaya  kufuatia kuchapwa usiku wa jana na FC Barcelona.

Msimu uliopita wakiwa na Ancelotti, Napoli ilikuwa miongoni mwa timu ambazo zilikuwa zikiwania ubingwa wa Serie A. Katika moja ya mahojiano yake ya hivi karibuni, aliwahi kuulizwa kocha huyo kuwa anampango wa kuachia ngazi kufuatia mwenendo mbovu wa klabu hiyo?

Ancelotti alisema hajawahi kufanya hivyo katika maisha yake yote ya ufundishaji soka.