Beki Aggrey Morris wa Azam afiwa na mkewe

Saturday January 11 2020
Morrispic

Dar es Salaam.Nahodha wa Azam FC, Aggrey Morris, amepata pigo zito baada ya kufiwa na mkewe wakati akijifungua usiku wa leo Jumamosi, jijini Dar es Salaam.

Msiba huo umetokea muda mfupi baada ya kumalizika kwa pambano la nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi 2020, iliyoihusisha timu yake ya Azam dhidi ya Simba na watetezi hao kupoteza kwa mikwaju ya penalti 3-2 baada ya suluhu ya dakika 90.

Aggrey, ambaye pia ni nyota wa timu ya taifa, Taifa Stars hakuwepo kwenye kikosi cha timu yake kilichokuwa Zanzibar kwa michuano hiyo kwani alikuwa akimuuguza mkewe aliyekuwa mjamzito.

Kupitia ukurasa wao wa Instagram klabu ya Azam imetoa taarifa juu ya msiba huo kwa kusema;

"Azam FC tumepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mke wa nahodha wetu, Aggrey Morris, aliyefariki dunia jana jioni wakati akiwa kwenye harakati za kujifungua.

Tunatoa salamu zetu za pole kwenda kwa familia ya Morris, pamoja na ndugu, jamaa na marafiki na wote walioguswa na msiba huo.

Advertisement

Azam FC tunaungana na familia ya marehemu na tunamuomba Mwenyezi Mungu, awajalie nguvu na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.

Bwana ametoa na Bwana Ametwaa, Jina lake lihimidiwe. Amen."

Taarifa zaidi zinasema msiba upo nyumbani kwa mchezaji huyo, eneo la Kitunda Kinyantira, pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam.

Advertisement