Twiga Stars waichapa Algeria sasa yaisubiri Morocco

Sunday February 16 2020

Mwanaspoti, Twiga Stars, waichapa Algeria, Morocco, Tanzania, Mwanasport

 

By DORIS MALIYAGA

Dar es Salaam.Timu ya Taifa ya wanawake ya Tanzania 'Twiga Stars', kimeendeleza ubabe huko Tunisia baada ya kuichapa Algeria kwa mabao 3-2, katika mchezo uliopigwa leo Jumapili majira ya saa 8:00 mchana Uwanja wa Kram.

Mechi hiyo ni muendelezo wa mechi za mashindano yaliyoandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Kaskazini (UNAF).

Mabao ya Twiga Stars ya mchezo huo yalipachikwa na Mwanahamisi Omary aliyefunga mawili dakika ya 11 na za nyongeza baada ya 45 kumalizika, wakati la tatu na la ushindi lilitumbukizwa kimiani na Diana Lucas dakika ya 90.

Algeria wao walifunga mabao yao dakika ya 22, mfungaji akiwa Delligj Anissa na la pili dakika ya 45, lilipachikwa na Affak Horiya.

Kocha Mkuu Bakari Shime alisema: "Ulikuwa mchezo wa ushindani tunashukuru tumepata ushindi, tupo kwa ajili ya kujifunza na kujipanga kwa ajili ya mashindano mengine kwetu ni mashindano sahihi kwa maendeleo ya kikosi chetu."

Huo ni mchezo wa pili baada ya ushindi wa mechi ya kwanza ambayo waliichapa Mauritania mabao 7-0 Ijumaa iliyopita.

Advertisement

Baada ya mchezo huo, Tanzania inajiandaa na mchezo ujao keshokutwa Jumanne, dhidi ya Morocco. Mechi itachezwa katika uwanja huo wa Kram.

 

Advertisement