Simba SC kicheko! ITC ya Luis Miquissone yatua

Muktasari:

Simba ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara na ni vinara wa sasa wakiwa wamekusanya jumla ya pointi 50 kutokana na mechi 19, huku ikifunga mabao 42 na kuruhusu 10 langoni mwao.

Dar es Salaam.Mashabiki wa Simba wana kila sababu ya kutabasamu kwa sasa. Kwanza chama lao linaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa zaidi ya pointi 12 dhidi ya timu inayowafuata nyuma, lakini juzi kati ITC ya winga wao kipenzi, Shiza Kichuya ilishatua na usiku huu taarifa nyingine tamu imeingia.

Taarifa hiyo ni ile ya kuwasili kwa ITC ya winga mwingine mkali kutoka Msumbiji, Jose Luis Miquissone, hivyo kama Kocha Sven Vanderbroeck ataamua kumpanga keshokutwa Ijumaa dhidi ya JKT Tanzania ni yeye tu kwa sasa.

Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa jioni hii amethibitisha kutua kwa hati hiyo ya uhamisho ya kimataifa kutoka UD Songo aliyokuwa akiichezea kwa mkopo kutoka Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

"Ni kweli ITC ya Miquissone imeshatua jioni hii na hivyo yupo huru sasa kuitumikia timu, tumefurahi kwa sababu mashabiki walikuwa na hamu kubwa ya kumuona winga huyu akiitumikia timu yake," alisema Senzo.

Winga huyo ambaye amesajiliwa na Simba kwenye dirisha dogo ikiwa ni miezi michache tangu alipofanya shoo moja matata kwenye mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya timu yake ya zamani UD Songo na Simba zilizochezwa Msumbiji na jijini Dar es Salaam.

Katika mechi ya kwanza, Simba ililazimisha suluhu, lakini ikakubali sare ya 1-1 nyumbani na kung'olewa Raundi ya Awali kwa sheria ya bao la ugenini na kuchangia kutemeshwa kibarua kwa Kocha Patrick Aussems aliyekuwa akiinoa timu hiyo kipindi hicho.