Prime
Simba, Yanga vita 5 Ligi Kuu...

KATIKA siku ambayo wapenzi wa Ligi Kuu Bara watakuwa bize kufuatilia michezo ya ligi hiyo, basi ni kesho Jumapili zitakapochezwa mechi nane za raundi ya 30.
Katika mechi hizo, kuna vita tano zitapiganiwa kwa timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo ambapo baada ya hapo, itabaki mechi moja tu ya kiporo, itakayozihusu Yanga na Simba itakayofanyika Juni 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaa kuanzia saa 11:00 jioni.
Katika mechi za kesho, kuna vita ya kuwania ufungaji bora inayomuhusu kinara Jean Charles Ahoua wa Simba mwenye mabao 16, nyuma yake kuna Clement Mzize na Prince Dube wanaocheza Yanga wenye 13 kila mmoja sawa na Leonel Ateba wa Simba.
Pia Jonathan Sowah (Singida Black Stars) na Steven Mukwala (Simba) hawapo mbali kwani wamefunga mabao 12 kila mmoja. Pacome Zouzoua wa Yanga anayo 11 kama ilivyo kwa Gibril Sillah anayecheza Azam.
Kwa upande wa clean sheet, kipa wa Simba Moussa Camara anazo 18 akijihakikishia kumaliza kama kinara na anaweza kufikiwa na Djigui Diarra wa Yanga mwenye 16 ili wamalize kama makipa bora wawili wa msimu. Lakini Camara akipata clean sheet nyingine moja tu katika mechi mbili zilizobaki atakuwa ni mshindi pekee wa tuzo ya kipa bora.
Ukiachana tuzo hizo binafsi, upande wa timu tukianza na kule juu, Yanga yenye pointi 76, inapambana kutetea ubingwa wa ligi hiyo ikiicha Simba katika nafasi ya pili ikikusanya pointi 75. Zote zimecheza mechi 28, bado mbili, wakati timu nyingine zimeshuka dimbani mara 29 na kesho zinahitimisha.
Ukiweka kando vita ya ubingwa inayozihusu timu mbili, pia kila timu kwenye ligi hiyo inapiga hesabu za kumaliza katika nafasi nzuri kutokana na uwepo wa bonasi za mdhamini wa haki za matangazo ambapo kuna kibunda chake. Anayemaliza nafasi ya kwanza, bonasi anayopewa ni kubwa tofauti na wa nafasi ya pili, lakini pia hata aliyemaliza nafasi ya tatu hafanani na wa nne ingawa hapo mjadala ushafungwa, Azam imejihakikishia kumaliza ya tatu, Singida Black Stars ya nne. Kuanzia hapo kwenda chini, pia kila nafasi na fungu lake.
Mwisho kabisa, kuna timu mbili zimebaki kwenye wakati mgumu ambazo ni Tanzania Prisons na Namungo, huku Fountain Gate ikiwa tayari imekata tiketi ya kucheza mechi za mtoano (playoffs) kuepuka kushuka daraja. Kumbuka tayari KenGold na Kagera Sugar zimeshashuka daraja mapema.
Tanzania Prisons yenye pointi 30 katika nafasi ya 13 na Namungo iliyokusanya pointi 32 nafasi ya 12, ndizo zinazotolea macho zaidi mechi za kesho zitakapokuwa dimbani.
Fountain Gate yenye pointi 29, ikishinda dhidi ya Azam itafikisha pointi 32 ilizonazo Namungo hivi sasa lakini tofauti ya mabao itaifanya kuendelea kuwa chini, hivyo haitaepuka kuwepo katika nafasi mbili za kucheza playoffs ndiyo maana tunasema ile nafasi moja imeshawahiwa, imebaki nyingine kukamilisha hesabu.
Tanzania Prisons ikiifunga Singida Black Stars mechi ya mwisho, itafikisha pointi 33 ilizonazo Pamba Jiji ambayo yenyewe itakwenda kucheza dhidi ya JKT Tanzania.
Ili Tanzania Prisons ikae juu ya Pamba Jiji, inatakiwa iifunge Singida Black Stars, kisha Pamba Jiji ipoteze na tofauti ya mabao katika mechi hizo mbili iwe 9-0 faida kwa Prisons.
Namungo ambayo itaikaribisha KenGold katika mchezo wa mwisho, itakuwa katika wakati mgumu kwani licha ya wapinzani wao kushuka daraja, lakini inaweza kukutana na matokeo ya kushangaza kama ilivyokuwa dhidi ya Kagera Sugar zilipotoka 0-0 Jumatano wiki hii, hivyo inaweza kuangukia playoffs.
Wakati hayo yakisubiriwa, takwimu zinaonyesha hadi sasa msimu wa 2024-25 ukielekea ukingoni, zimechezwa jumla ya mechi 231 za Ligi Kuu Bara, bado tisa kukamilisha 240 huku kukiwa na rekodi mpya zimewekwa, huku nyingine zikiwa hazijavunjwa.
MABAO YA KUTOSHA
Msimu uliopita ilishuhudiwa hadi mwisho zilipochezwa mechi 240, yalifungwa jumla ya mabao 517, ambayo ukilinganisha na sasa, tayari yamevuka hali inayoonyesha msimu huu nyavu zimetikiswa sana. Kwa sasa katika mechi 231, yamefungwa mabao 544.
Ukiangalia katika msimu uliopita, wageni waliotikisa nyavu walikuwa 65 ambapo jumla yake walifunga mabao 206, huku wazawa 117 ndio waliofunga mabao 299. Hapa pia kuna mabao 12 ya kujifunga yanayokamilisha idadi hiyo kamili.
Ukija msimu huu, mabao 544 yamefungwa kwenye mechi 231, wageni waliotikisa nyavu ni 64 katika jumla ya mabao yao 235, huku wazawa waliofunga ni 115 katika mabao 292. Kumbuka kuna mabao 17 ya kujifunga yaliyokamilisha idadi hiyo ya mabao 544.
HAT TRICK KWA TOCHI
Licha ya kwamba msimu huu kuna mabao mengi yamefungwa kulinganisha na msimu uliopita, lakini suala la kupatikana hat trick limeonekana kuwa gumu zaidi.
Msimu uliopita hadi ligi inatamatika, zilipatikana hat trick saba zilizofungwa na Feisal Salum (Azam), Jean Baleke (Simba), Stephane Aziz Ki (Yanga) aliyefunga mara mbili, Kipre Junior (Azam FC), Wazir Junior (KMC) na Ismail Mgunda (Ihefu).
Msimu huu kuna hat trick nne tu, wafungaji ni Prince Dube (Yanga), Stephane Aziz KI (Yanga), Steven Mukwala (Simba) na Jean Charles Ahoua Simba).
UMEME NGOMA DROO
Ukija katika kadi nyekundu, hapa hadi sasa ngoma droo, ingawa kuna mechi za kuchezwa zimebaki, tusubiri tuone kwani lolote linaweza kutokea.
Msimu uliopita zilionyeshwa kadi nyekundu 21 katika mechi 240, msimu huu zikiwa zimechezwa mechi 231, pia kadi nyekundu 21 zimetoka.
PENALTI ZA KUMWAGA
Wakati msimu uliopita zikipigwa penalti 48 huku Saido Ntibazonkiza aliyekuwa Simba akiongoza kwa kupiga saba akifuatiwa na Stephane Aziz KI aliyeondoka Yanga hivi karibuni aliyekuwa nazo tatu, msimu huu hadi sasa zimepigwa 87, bado kidogo ziwe mara mbili yake. Kinara wa penalti msimu huu ni Leonel Ateba wa Simba aliyepiga saba akifuatiwa na Jean Charles Ahoua (Simba) na Stephane Aziz Ki (Yanga) waliopiga sita kila mmoja.
REKODI CLEAN SHEET IMEVUNJWA
Aliyekuwa kipa wa Coastal Union, Ley Matampi msimu uliopita alimaliza kinara wa clean sheet akiwa nazo 15, akifuatiwa Djigui Diarra (Yanga) aliyemaliza na 14. Chini yao walikuwa Constatine Malimi (Geita Gold), Jonathan Nahimana (Namungo) na Ayoub Lakred (Simba) ambao kila mmoja alikusanya 10.
Msimu huu, Moussa Camara wa Simba amejihakikishia kumaliza kinara akiwa nazo 18 na mtu pekee anayeweza kumfikia pale kileleni ambapo hakuna wa kumng’oa ni Djigui Diarra (Yanga) aliyekusanya 16. Camara anaweza kumaliza kinara pekee, kama atapata angalau clean sheet moja zaidi katika mechi mbili zilizobaki.
AZAM WAKALI WA ASISTI
Kwa msimu wa pili mfululizo, inaonekana nyota wa Azam kuwa wakali wa kutengeneza mabao kwani msimu uliopita Kipre Junior alimaliza kinara wa asisti akiwa nazo tisa, akifuatiwa na Stephane Aziz KI (Yanga) aliyemaliza na nane, huku Feisal Salum (Azam), Yao Kouassi (Yanga) na Clatous Chama (Simba) kila mmoja akipiga saba.
Msimu huu, pia nyota wa Azam anaongoza ambaye ni Feisal Salum mwenye 13, kwa hali ilivyo, kuna asilimia kubwa akamaliza kinara kwani anayefuatia ni Maxi Mpia Nzengeli (Yanga) na Jean Charles Ahoua (Simba) ambao kila mmoja anazo tisa, huku Pacome Zouzoua (Yanga), Josephat Arthur Bada (Singida Black Stars) na Prince Dube (Yanga) kila mmoja akiwa nazo nane.
WASIKIE MAKOCHA
Kuelekea mechi za uamuzi, kocha msaidizi wa Namungo, Ngawina Ngawina, alisema matokeo waliyoyapata dhidi ya Kagera Sugar ni sehemu ya mchezo, kwani waliingia bila ya kuwaheshimu wapinzani wao, hivyo hawatarajii makosa hayo yajirudie watakapocheza dhidi ya KenGold.
“Wengi walitarajia tutapata matokeo mazuri na kujiweka katika nafasi nzuri ya kujihakikishia kucheza msimu ujao tukikwepa presha iliyopo sasa, lakini makosa tuliyoyafanya hayawezi kujirudia, tunajiandaa kuhakikisha tunautumia vyema uwanja wa nyumbani na kuwahakikishia wana Ruangwa kuwa msimu ujao tutashiriki Ligi Kuu,” alisema Ngawina.
Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Aman Josiah alisema makosa binafsi kwa wachezaji wake ndio yamewapa matokeo ya kufungwa 5-0 na Yanga katika mchezo uliopita, akieleza kuwa hata hivyo ubora wa wapinzani wao ulichangia kipigo hicho.
Alisema kwa sasa wanakwenda kupambana ugenini kuona wanamaliza vipi msimu huku matarajio ni kutoangukia katika mechi za playoffs kwani huko lolote linaweza kutokea.