Sillah achekelea mabao 11 Bara

Muktasari:
- Nyota huyo raia wa Gambia anayeitumikia Azam kwa msimu wa pili, mapema alinukuliwa na Mwanaspoti kwamba anatamani kufunga mabao 10 ili kuvuka rekodi ya msimu uliopita aliomaliza na manane na wakati kesho ligi ikifikia tamati ameshafunga 11 baada ya Jumatano kufunga mawili katika ushindi wa 5-0 dhidi ya Tabora United kabla ya kesho kumalizana na Fountain Gate.
NDOTO ya mshambuliaji wa Azam FC, Gibril Sillah kumaliza msimu akifunga mabao yasiyopungua 10 imetimia, na akasema ni kitu ambacho kimemuongezea thamani kwenye wasifu kucheza soka Tanzania.
Nyota huyo raia wa Gambia anayeitumikia Azam kwa msimu wa pili, mapema alinukuliwa na Mwanaspoti kwamba anatamani kufunga mabao 10 ili kuvuka rekodi ya msimu uliopita aliomaliza na manane na wakati kesho ligi ikifikia tamati ameshafunga 11 baada ya Jumatano kufunga mawili katika ushindi wa 5-0 dhidi ya Tabora United kabla ya kesho kumalizana na Fountain Gate.
Akizungumza na Mwanaspoti, Sillah alisema katika nafasi anayocheza kiwango chake kinapimwa na ufungaji wa mabao, jambo alilofanikiwa kwa kiasi kikubwa huku akiwa na matarajio ya kuongeza mabao zaidi katika mechi ya mwisho dhidi ya Fountain Gate itakayopigwa kesho. “Safari ya msimu huu ilikuwa ngumu na yenye ushindani wa juu, ninachofurahia ndoto yangu imekuwa halisi katika nafasi ninayocheza inayopimwa kwa kufunga mabao mengi natamani mechi ya mwisho kama nitapangwa nifunge zaidi,” alisema Sillah mwenye asisti mbili pia.
“Msimu wangu wa kwanza nilimaliza na mabao manane baada ya kupata uzoefu wa kujua Ligi ya Tanzania ipo tafu na inahitaji kutumia nguvu na akili kubwa nikatamani idadi ya mabao iongezeke na hilo limekuwa.”
Baadhi ya timu ambazo Sillah alizifunga msimu wa 2023/24 ambao alimaliza na mabao manane na asisti sita ni Yanga 3-2, Azam 2-1 Yanga, Azam 5-0 KMC, Azam 4-0 KenGold, Mashujaa 0-3 Azam, Mtibwa Sugar 0-2 Azam.
Alisema ndani ya misimu miwili amejifunza mengi na amefurahia kuona wachezaji kadri muda unavyokwenda ndivyo wanavyozidisha ushindani. “Ligi inakuwa hamasa ya kuongeza kiwango kila mechi, ukicheza inakuwa ngumu inatakiwa inayokuja mbele yako ujipange zaidi, hilo ni jambo zuri kwa mchezaji.”