Mwamba mpya wa Man Utd anayempa Solskjaer kiburi

Saturday October 17 2020

 

MANCHESTER, ENGLAND. MMOJA kati ya wachezaji waliosajiliwa na Manchester United katika dirisha la usajili lililopita ni huyu mwamba Alex Telles, ambaye anatarajiwa kufanya makubwa kwa msimu huu.

Telles, ambaye alisajiliwa kwa dau la Pauni 18 milioni, ni miongoni mwa wachezaji waliokuwa wanawindwa na Man United kwa muda mrefu kutokana na kiwango alichoonesha katika msimu uliopita akiwa na FC Porto.

Mwanaspoti inakuletea historia ya maisha halisi ya mwamba huyu kutoka Brazil kuanzia alipozaliwa hadi hapo alipofikia.

Telles ni nani?

Jina lake ni Alex Nicolao Telles, amezaliwa 1992 na baba yake Jose Telles sambamba na mama yake Claudete Telles huko Caxias do Sul nchini Brazil.

Katika familia yao walikuwa ni watoto wawili akiwa yeye na dada yake aitwaye Moreso, ambaye ni mkuwa zaidi yake.

Advertisement

Katika ukuaji wake jamaa alikuwa anasifika zaidi kwenye sekta ya kukimbia, kipaji hicho cha kukimbia kilikuwa kinaonekana alipokuwa anashindana na rafiki zake ambao, walikuwa wanaambulia patupu wanapojaribu kumkimbiza na hiyo ilisababisha abatizwe jina la Usain Bolt.

Hali ya kiuchumi ya familia yake ilikuwa ni ya kawaida, kipato cha wazazi wake kilikuwa kinatosha kulisha familia na mahitaji mengine muhimu.

Safari yake kISOKA

Hakuwahi kuwa na ndoto za kucheza soka hadi alipofikisha miaka minane ambapo, rafiki zake ambao walikuwa wanacheza mpira katika mtaa wao, walimshawishi hivyo naye akaanza kucheza huko mpaka mwaka 2007 ambapo, alijiunga na akademi ya timu ya Esporte Clube Juventude ambapo alionekana kama ni mmoja kati ya wachezaji wenye vipaji vikubwa kutokana na kasi yake na ufundi wake anapokuwa na mpira mguuni.

Alipofikisha umri wa miaka 18, mwaka 2010 alipandishwa kikosi cha kwanza cha timu ya Juventede ambapo alifanikiwa kuiwezesha timu hiyo kushinda taji la Copa FGF.

Mwaka 2012 alisajiliwa kwenda Gremio ambapo alichukua tuzo ya beki bora wa kushoto kwa misimu mfululizo kabla ya Galatasaray mwaka 2014 ambapo, alikaa kwa misimu miwili na akaiwezesha kushinda taji la Ligi Kuu, Turkish Cup na Turkish Super Cup.

Baada ya kuonesha kiwango kikubwa akiwa na miamba hiyo mwaka 2015, timu nyingi barani Ulaya zilionesha nia ya kutaka kumsainisha na zaidi ilikuwa Chelsea ambayo ilikuwa inataka kumfanya kuwa mbadala wa Felipe Luis lakini dili lilifeli na ikasababisha atolewe kwa mkopo kwenda Inter Milan ambapo alikaa kwa msimu mmoja kabla ya kujiunga na FC Porto kwa dau la Euro 6 milioni.

Baada ya kujiunga na Porto aliendelea kuonesha moto na ameshinda tuzo kadhaa za beki bora sambamba na makombe ikiwa pamoja na lile Ligi Kuu.

Maisha binafsi

Jamaa ameoa mwaka 2018 na mkewe anaitwa Priscila Minuzzo kwa sasa ana umri wa miaka 27, lakini haijajulikana ikiwa ana mtoto au la kwani, si mtu wa kuweka mambo yake hadharani.

 

Advertisement