Mukoko anapowarudisha darasani Mauya, Makame

Thursday September 10 2020

 

By KHATIMU NAHEKA

KUNA kitu kinaonekana kuingia kama mabadiliko katika kikosi cha Yanga baada ya usajili wao mkubwa katika kuboresha timu yao ambayo imepotea katika mbio za kuchukua mataji kwa muda wa miaka mitatu sasa.

Kuna watu wapya wameingia katika kikosi chao ambao kwa mbali kuna kitu kipya kinaonekana ambacho ni muda tu utaamua kwamba ujio wa watu hao na mwanzo wao kama utaweza kuisaidia timu hiyo kufikia malengo yake katika msimu huu mpya.

Mojawapo wa nyota walioingia ndani ya timu hiyo ni kiungo Mukoko Tonombe akitokea pale AS Vita ya DR Congo katika Jiji la Kinshansa tena akiwa mchezaji muhimu katika timu hiyo.

Mukoko ameichezea Yanga kwa takriban kama robo saa tu katika mechi ya ligi iliyopita, lakini ukichukua alichofanya unaweza kuamua kuingia darasani na kujifunza hasa kwa wale ambao wanataka kuona ubora wa kiungo mkabaji.

Muangalie Mukoko anachofanya uwanjani, anaonekana anajua majukumu yake vyema.

Kwanza akili yake muda mwingi anawaza kukaba - tena akiwa katika eneo lake mbele kidogo ya mabeki wa kati akienda kulia na kushoto.

Advertisement

Kuna wakati utamuona anaamua kusogea juu ingawa hili huwa halifanyi mara kwa mara na akishafanikiwa kuunasa mpira kazi yake inakuwa moja tu, kutafuta nani au wapi apeleke huo mpira ikiwa ni akili ya kuanzisha mashambulizi. Hilo pia ni jukumu lake kubwa.

Jifunze pia ubora wake wa kupiga pasi na hata jicho lake la kujua wapi anatakiwa kuupeleka mpira na uzuri ni kwamba anajua katika timu yake kuna watu wana mbio, kwa hiyo haraka anaanza kutafuta wapi alipo mtu anayekimbia.

Huyu sio mtu wa kupaka rangi kila wakati na kutaka aonekane anapiga visigino kama ambavyo viungo wetu walivyo, lakini pia sio mtu wa pasi za kulia na kushoto (square pass).

Mara nyingi anataka kuona pasi zake zinakwenda mbele kuanzisha mashambulizi.

Kingine muhimu ni jitihadi zake, lakini anavyopenda kuwahamasisha wenzake kucheza kwa kujituma uwanjani na kuacha kucheza kwa kupunguza kasi ni mtu muhimu kuwarudisha wenzake mchezoni.

Kuna mambo hapa naona kuna haja wachezaji wetu kama viungo Zawadi Mauya na hata Abdulaziz Makame wanaweza kujifunza kwa utulivu kupitia kazi anayoifanya Mukoko anapokuwa kama kiungo mkabaji.

Shida kubwa ya viungo wetu wakabaji wanataka kufanya mambo mengi ambayo yako nje ya majukumu yao, na hapo ndipo wanapojikuta wanaharibu na kupoteza kuaminiwa na makocha kwa kupewa majukumu ya eneo hilo.

Ukiangalia mtu kama Makame ni mmoja kati ya viungo bora, lakini anapokuwa akicheza kama kiungo mkabaji kuna mambo mengi anataka kuyafanya ambayo mwisho wa siku yanamfanya kuharibikiwa na hata kuweza kuiweka timu katika wakati mgumu.

Makame anatakiwa kuvuna utulivu wa Mukoko na pia ubora wa kuunasa mpira na kuachia pasi kwa haraka na hata kupiga pasi ndefu zinazofika, kwa kuwa tayari ameshajaliwa nidhamu ya kukaba kwa nguvu na kupenda kupambana akiwa uwanjani.

Anapotaka kufanya vitu vya ufundi kama Haruna Niyonzima au wakati mwingine kuwa kama swahiba wake, Feisal Salum, hapo ndipo anabadilika na kutokuwa Makame tena na kuharibikiwa kabisa na ikifikia hapo kocha hawezi kukuamini tena.

Eneo la kiungo mkabaji ni la hatari sana endapo atapewa nafasi mchezaji ambaye hatakuwa na ubora wa kupiga pasi zinazofika.

Ukiwa na mtu ambaye anapoteza mipira vibaya inaweza kuwa ni kama kuwatengenezea nafasi washindani wako na hapo ndipo hatari inapokuja.

Kuna wakati wachezaji wanaweza kujifunza kupitia ubora walionao wenzao na hapa ndipo ninapoona kuwepo kwa haja ya viungo wengi wakabaji kujifunza kupitia ubora wa Mukoko anachofanya anapokuwa uwanjani.

Darasa la mkali huyu wa kiungo halipaswi kuishia kwa kina Mauya na Makame pekee, bali kwa viungo wa timu zetu zote.


Advertisement