Muhiddin ashtukia tatizo Bandari

Muktasari:

Hapo ndipo uamuzi wa kumpa jukumu hilo Muhiddin likaafikiwa. Hata hivyo, naye huenda yakawa ni yale yale kama tu ya Mwalala, ikiwa matokeo ya wikendi walipocheza dhidi ya Gor kule Nakuru, kwenye mechi ya ligi kuu ni jambo la kuzingatiwa.

LICHA ya kuanza kazi kwa kupokezwa kipigo kizito cha mabao matatu mtungi na Gor Mahia, kocha wa muda wa Bandari FC Twahiri Muhiddin kasisitiza imebadilika kwa sasa.

Muhiddin aliyewahi kuifunza Bandari awali, alipewa majukumu ya kuisimamia timu wiki mbili zilizopita kutoka kwa Kocha Bernard Mwalala aliyeombwa akae kando kidogo.

Hatua hiyo ilijiri baada ya msururu wa matokeo mabovu kuendelea chini ya Mwalala na matumaini yakawa ni pengine chini ya kocha mwingine, mambo yatabadilika.

Hapo ndipo uamuzi wa kumpa jukumu hilo Muhiddin likaafikiwa. Hata hivyo, naye huenda yakawa ni yale yale kama tu ya Mwalala, ikiwa matokeo ya wikendi walipocheza dhidi ya Gor kule Nakuru, kwenye mechi ya ligi kuu ni jambo la kuzingatiwa.

Katika mechi hiyo Bandari walilemewa mwanzo mwisho na wala hawakuonekana kuwa makini. Lakini licha ya kichapo hicho kizito, Muhiddin kasisitiza mchezo wao umebadilika kabisa ila tatizo lipo tu kwenye ufungaji.

“Tulikosa zaidi ya tatu sisi (mabao). Tulitengeneza mabao mengi sana tukakosa. Ni ufungaji tu ndio tumeshindwa lakini nimefurahishwa na mabadiliko ya mchezo wetu,” Muhiddin kasema.

Sasa zikiwa zimesalia mechi 15, msimu huu kufikia kikomo, Muhiddin angali ana muda wa kuthibitisha kauli yake kuwa mchezo wao umebadilika.