Msuva: Hakuna mwenye uhakika wa namba Stars

Muktasari:

Taifa Stars imepangwa Kundi C na inatarajiwa kutupa karata ya kwanza dhidi ya Senegal, Juni 23, kabla ya kuivaa Kenya Juni 27 na kumaliza Julai 3 na Algeria

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’, Saimon Msuva   amesema hakuna mchezaji  mwenye uhakika wa namba katika kikosi cha kwanza.

Taifa Stars imepiga kambi Misri kujiandaa kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), zilizopangwa kuanza Juni 21 hadi Julai 19, mwaka huu.

Mshambuliaji huyo wa Difaa El Jadida ya Morocco, alisema Kocha Emmanuel Amunike amewaeleza hana kikosi cha kwanza.

Msuva alisema mara kwa mara Amunike amekuwa akiwataka kila mmoja kufanya mazoezi kwa bidii kwa kuwa atapanga kikosi kulingana na kiwango bora cha mchezaji.

“Mara kwa mara kocha amekuwa akisisitiza kabla na baada ya mazoezi kwamba hatajali umaarufu wa mchezaji au jina la mtu, zaidi ataangalia unafanya nini katika mafunzo yake,” alisema Msuva akimnukuu Amunike.

Kauli ya Msuva imekuja wakati Taifa Stars ikijiandaa kwa mchezo wa kirafiki utakaochezwa Alhamisi kwenye Uwanja wa Borg El Arab, Alexandria dhidi ya Misri.

“Uzuri wa kocha ni muwazi, mchezaji yeyote anaweza kumpa nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza kwa kigezo kimoja tu ambacho ni uwajibikaji wake kuanzia kwenye mazoezi, nidhamu ndani na nje ya uwanja,” alisema nyota huyo wa zamani wa Yanga.

Alisema kauli ya Amunike imekuwa ikichochea kila mmoja kufanya mazoezi kwa nguvu kwa lengo la kupata namba katika kikosi cha kwanza kwenye fainali hizo.

Nyota huyo aliyefunga mabao 13 katika kikosi cha Difaa El Jadida msimu uliopita, alisema morali ya wachezaji ipo juu na wameridhika na mafunzo wanayopata  chini ya Amunike.

Msuva alisema wamekuwa wakifanya mazoezi ya kujenga utimamu wa mwili na muda mrefu wanajikita katika mbinu mbalimbali za kiufundi.

Nyota Rashid Mandawa anayecheza soka nje katika klabu ya BDF XI  ya Botswana, alisema mafunzo wanayopata ya kiwango cha juu na hali ya hewa ni sawa na Tanzania.

Mandawa alidokeza wamejiandaa kupambana katika fainali hizo ambazo Taifa Stars inashiriki kwa mara ya pili baada ya kupita miaka 39.

Mara ya mwisho Taifa Stars kucheza fainali hizo ilikuwa mwaka 1980 mjini Lagos, Nigeria.

Taifa Stars imepangwa Kundi C na inatarajiwa kutupa karata ya kwanza dhidi ya Senegal, Juni 23.