Mshtuko,David De Gea afuata njia ya Ramsey

Muktasari:

Juventus haijafanya siri kwamba inamtaka kipa huyo wa kimataifa wa Hispania kwa ajili ya kuchukua nafasi ya kipa wake wa kwanza, Wojciech Szczesny na haitakuwa mara ya kwanza kunasa wachezaji mahiri wakiwa huru.

MANCHESTER, ENGLAND.NJIA ni ileile tu. Wataalamu wa kupata mastaa wa bure, Juventus wamerudi tena katika njia yao na wanataka kufungua maongezi na kipa wa Manchester United, David de Gea kwa ajili ya kumpa mkataba wa awali dirisha la Januari.

De Gea amekwamisha mazungumzo ya mkataba mpya Old Trafford licha ya klabu hiyo kuweka mezani dau la mshahara la Pauni 350,000 ambalo litamfanya awe mchezaji anayelipwa zaidi klabuni hapo.

Kipa huyo amewaambia marafiki zake anataka kuondoka mwishoni mwa msimu kama mchezaji huru na Juventus inaamini itampata staa huyo bure huku United ikishindwa kuambulia chochote.

Juventus haijafanya siri kwamba inamtaka kipa huyo wa kimataifa wa Hispania kwa ajili ya kuchukua nafasi ya kipa wake wa kwanza, Wojciech Szczesny na haitakuwa mara ya kwanza kunasa wachezaji mahiri wakiwa huru.

Mastaa ambao Juventus imewanasa bure kwa kipindi cha miaka 15 iliyopita ni pamoja na Fabio Cannavaro, Paul Pogba, Andrea Pirlo, Fernando Llorente, Kingsley Coman, Sami Khedira, Dani Alves, Emre Can pamoja na Aaron Ramsey na Adrien Rabiot ambayo iliwanasa katika dirisha kubwa lililopita la majira ya joto.

Inajulikana kwa muda mrefu PSG ya Ufaransa pia inamtaka De Gea lakini Juventus kwa sasa inaongoza katika mbio za kumchukua kama ataamua kuondoka Old Trafford wakati huu United ikianza kusaka makipa wa kuchukua nafasi yake.

Inadaiwa mabosi wa United wameanza kumnyemelea kipa wa kimataifa wa Slovenia, Jan Oblak anayetamba katika lango la Atletico Madrid ya Hispania kwa ajili ya kuchukua nafasi ya De Gea ambaye pia ilimchukua kutoka Atletico katika dirisha kubwa la mwaka 2011 kwa dau la Pauni 17 milioni.

Hii ni mara ya pili kwa De Gea kukaribia kuondoka Old Trafford ambapo mwaka 2015 alikuwa katika dakika za mwisho kutua katika Klabu ya Real Madrid kabla ya uhamisho huo kuvurugika dakika za mwisho kwa kile kilichoelezwa kukorofisha kwa faksi ya mawasiliano.

Baada ya Madrid kuendelea kumfukuzia De Gea kwa muda mrefu hatimaye iliachana na mpango huo na katika dirisha kubwa la mwaka jana iliamua kumchukua kipa wa kimataifa wa Ubelgiji, Thibaut Courtois kutoka Chelsea na tangu hapo imeachana na De Gea.

Julai mwaka huu, Kocha wa Manchester United, Old Gunnar Solskjaer alionyesha matumaini ya kipa huyo kusaini mkataba mpya klabuni hapo lakini mpaka sasa mchakato huo haujazaa matunda na De Gea anakuwa katika majaribu ya kuondoka bure.

“David alikuwa katika mapumziko huku akizungumza kuhusu mkataba mpya mpya na pia kuufikiria, kwahiyo tuna matumaini tutatatua suala hilo. Najiamini. Kuhusu David nimesema mara nyingi jinsi gani nilivyo na bahati, na jinsi tulivyo na furaha, kuwa naye katika lango. Nina matumaini atabakia hapa kwa miaka mingi,” alisema Soslkjaer wakati huo.

Endapo De Gea ataondoka na United itafanikiwa kumnasa Oblak bado pengo lake halitakuwa kubwa sana kutokana na kiwango cha kusuasua cha De Gea katika miezi ya karibuni huku Oblak akiwa mmoja kati ya makipa bora duniani tangu atue Atletico mwaka 2014.

Ameichezea Atletico mechi 156 za La Liga na kuruhusu mabao 96 tu huku akizuia nyavu zake zisiguswe katika mechi 90 na kuokoa michomo 385 katika asilimia 79.8.