Mrundi aitwa kuokoa jahazi Azam FC

Muktasari:

Azam FC inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 54 ilizokusanya kwa kushinda michezo 16, kutoka sare mara sita na kupoteza mechi sita.

Uwezekano finyu wa kocha Aristica Cioaba kurejea nchini kwa wakati umeufanya uongozi wa Azam FC kumuita haraka nchini kocha, Vivier Bahati kutoka Burundi kuja kuongoza benchi lao la ufundi hadi katika mechi zilizosalia za Ligi Kuu.

Uamuzi huo wa Azam FC umekuja mara baada ya serikali kutangaza utaratibu wa namna ligi kuu, ligi daraja la kwanza, ligi daraja la pili na Kombe la Azam Sports Federation zitakavyochezwa mara baada ya shughuli za michezo kurejeshwa nchini

Mkuu wa idara ya habari na mawasiliano ya Azam FC, Thabit Zakaria alisema kuwa Vivier atalazimika kuliongoza benchi la ufundi kwa mechi zilizobakia za Ligi Kuu na Kombe la Azam Sports Federation kwa vile Cioaba amekwama huko Romania.

Zakaria alisema kuwa Romania ni miongoni mwa mataifa ambayo yameweka sheria ya raia wake kukaa ndani kama hatua za kukabiliana na virusi vya Corona lakini pia hata shughuli za usafiri wa anga zimesimama.

"Kocha mkuu kule Romania hawezi kupatikana hivi karibuni kwa hiyo njia pekee tuliyoifanya ni kumuwezesha kocha Msaidizi Vivie Bahati ambaye yuko Burundi atarudi Jumapili hii atakuwa safari kurudi hapa.

Na unajua ndege za kimataifa hazijaanza kwenda kule wala kutoka. Lakini Burundi sio mbali na Tanzania kwa hiyo atakuja kwa usafiri wa gari kutoka Burundi hadi maeneo fulani ya karibu mpakani kati ya Kigoma au Kagera kutegemeana na njia atakayopata.

Halafu pale ndio apande ndege kuja Dar es Salaam kuendelea na majukumu mengine. Yeye atakaimu nafasi ya ukocha mkuu na kocha wa makipa, Iddi Abubakar atakuwa msaidizi wake wakisaidiana na meneja wetu, Luckson Kakolaki," alisema Zakaria

Mbali na Cioaba, Azam pia inaweza kuwakosa nyota wake saba walio nje ya nchi ambao ni Yakub Mohamed, Daniel Amoah na Razack Abalora (Ghana), Never Tigere, Donald Ngoma na Bruce Kangwa (Zimbabwe) na Nicholas Wadada (Uganda) ambao nchi zao pia kumewekwa sheria hiyo.