Molinga, Kagere wafunika mbaya

Muktasari:

Moro ndiye mchezaji pekee wa kigeni mpaka sasa aliyejifunga bao, kwani nyota wengine nane waliotupia kambani kwao ni wazawa.

WAKATI jumla ya mabao 406 yakifungwa katika mechi 207 za Ligi Kuu Bara, nyota wa kigeni wakiongozwa na Meddie Kagere wa Simba David Molinga wa Yanga sasa na Obrey Chirwa wa Azam wamefunika bovu kwa kasi yao ya kufumania nyavu na kutoa mchango mkubwa kwa timu zao.

Licha ya kwamba wazawa wametumia faida ya wingi wao kuzifungia mabao timu zao, lakini ukweli wageni pamoja na uchache wao, wameonekana bado wana faida kubwa vikosini kwa kutupia kambani mpaka sasa ligi ikiwa kwenye raundi ya 21.

Wachezaji wazawa wamefunga zaidi ya robo tatu ya mabao yote hayo wakiwa wamefumania nyavu mara 328 sawa na 80.55% huku wachezaji wazawa wakiwa wamefunga mabao 79 tu ambayo ni sawa na 19.45% tu.

Katika hali ya kushangaza, wakati kukiwa na kundi la zaidi ya wachezaji 65 wa kigeni wanaozichezea na waliowahi kuzichezea timu mbalimbali za Ligi Kuu Tanzania Bara, ni nyota 30 tu walioweza kufumania nyavu, huku mmoja Lamine Moro akijifunga langoni mwake na wengine wakitoka kapa.

Moro ndiye mchezaji pekee wa kigeni mpaka sasa aliyejifunga bao, kwani nyota wengine nane waliotupia kambani kwao ni wazawa.

KAGERE, MOLINGA, CHIRWA NOMA

Hapana shaka, Kagere ndiye ameonekana kuwabeba zaidi wenzake katika kundi hilo akiwa amefunga mabao 12 kati ya hayo 78 yaliyofungwa na wageni huku yaliyobakia 66 yakifungwa na wengine.

Mabao ya Kagere ni sawa na asilimia tatu ya mabao yote yaliyofungwa katika Ligi Kuu na hakuna mchezaji yeyote wa ligi hiyo iwe mzawa au mgeni ambaye amechangia kwa kufunga idadi kubwa ya mabao.

Molinga wa Yanga anayetokea DR Congo na Mzambia Obrey Chirwa wa Azam, ndio wanaomfuatia Kagere kwa kufumania nyavu, kila mmoja akipachika mabao saba katika Ligi Kuu sawa na 1.75%.

WAGENI SIMBA SALUTI

Simba inaweza kujivunia zaidi usajili wake wa mapro wa kigeni kwani nyota wake wamepachika idadi kubwa ya mabao katika ligi hiyo msimu huu kuliko klabu nyingine yoyote.

Nyota saba wa kigeni wameifungia Simba mabao 26 sawa na 6.48% ya mabao yote yaliyofungwa katika Ligi Kuu ambapo Kagere aliyepachika mabao 12, Deo Kanda (4), Francis Kahata (3), Gerson Fraga (3), Clatous Chama (2) na Sharaf Shiboub na Tairone Santos ambao kila mmoja amepachika bao moja

Ikumbukwe kwamba hadi sasa kiujumla Simba imefunga mabao 45 sawa na 60% ya mabao yote iliyofunga hivyo wageni wamefunga zaidi ya nusu ya mabao hayo wakati mengine 19 yakifungwa na wazawa ambayo ni sawa na 40% tu.

Wanaofuatia kwa kunufaika na mabao ya wageni ni Yanga waliofunga 17 sawa 2.24% ya mabao yote katika Ligi Kuu, huku Molinga akiwa kinara wao akipachika saba, Patrick Sibomana (4), David Morrison (2) huku Sadney Urikhob, Juma Balinya, Haruna Niyonzima na Yikpe Gnamien kila mmoja akipachika bao moja kati ya mabao 24 ya timu yao.

Idadi hiyo ya mabao yote ya Yanga inaonyesha yamechangiwa na wageni kwa 70.83% , huku Azam yenyewe, katika mabao 28 iliyofunga, wageni sita wamefumania nyavu mara 15 sawa na 53.57%.

Idadi hiyo ya mabao 15 ya Azam FC yaliyofungwa na wageni ni sawa na 3.74% ya mabao yote yaliyofungwa hadi sasa.

Mapro wa Azam waliofumania nyavu katika mara hizo 15 ni Chirwa mwenye mabao saba, Richard Djodi (3), Donald Ngoma (2) wakati Daniel Amoah, Nicolas Wadada na Yakub Mohamed kila mmoja akifunga bao moja.

FRAGA APIKU REKODI YA JAJA

Kitendo cha kiungo wa Simba, Gerson Fraga kupachika mabao matatu katika Ligi Kuu imemfanya awe raia wa Brazil na Amerika ya Kusini aliyepachika idadi kubwa zaidi ya mabao nchini.

Awali rekodi hiyo ilikuwa inashikiliwa na Gerson Santos ‘Jaja’ ambaye alipachika mabao mawili katika ligi hiyo.

MATAIFA 13 YAWEKA ALAMA

Mabao hayo 79 ambayo yamefungwa na wageni katika Ligi ya msimu huu, yamepachikwa na nyota 30 kutoka katika mataifa 13 tofauti.

Mataifa hayo ni DR Congo, Rwanda, Kenya, Uganda, Sudan, Ghana, Nigeria, Ivory Coast, Zambia, Zimbabwe, Namibia, Brazil na Burundi.

Rekodi zinaonyesha Rwanda, DR Congo ndizo zinatikisa, kwani Wanyarwanda wamefumania nyavu mara 18 sawa na 4.49% ya mabao yote ya Ligi Kuu.

Wachezaji hao wa Rwanda ni; Kagere (12), Sibomana (4) na Haruna Niyonzima na Jean-Baptiste Mugiraneza ambao kila mmoja kafumania nyavu mara moja.

DR Congo inafuata kwa wachezaji wake, Molinga na Deo Kanda kwa pamoja wamepachika mabao 11. Molinga akifunga saba na Kanda akifunga manne.

Zambia wanashika nafasi ya tatu ambapo wachezaji wake wamefumania nyavu mara 10, Nigeria (7), Burundi (7), Ghana (6), Ivory Coast (6), Brazil (4), Kenya (3), Uganda (2), Zimbabwe (2) wakati Namibia na Sudan wachezaji wao wamefumania nyavu mara mojamoja.

MSIKIE MGOSI

Kasi hiyo ya nyota wa kigeni imemfanya straika wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Mussa Hassan Mgosi anasema uwepo wa mapro wa kigeni una mchango mkubwa kwani hata katika Tano Bora ya Wafungaji wamejaza wao na wakiwa na mabao ya kutosha.

“Licha ya kuwepo kwa mipango ya kutaka kuona idadi ya wageni inapungua, lakini ukweli wana mchango mkubwa na kusaidia kuwapa changamoto wazawa, kama watapungua inaweza kufanya wachezaji wa Kitanzania kuzubaa tofauti na sasa wanachangamshwa,” alisema Mgosi.

Mgosi alisema kitu ambacho anadhani kinapaswa kufanywa kwa sasa na wazawa ni kuamka kutoka usingizini na kupambana ikiwezekana msimu huu warejeshe kiatu cha dhahabu cha Mfungaji Bora ambayo kwa misimu miwili mfululizo kinashikiliwa na wageni.