Molinga apiga bao Yanga yainyuka Mtibwa Sugar

Muktasari:

Ushindi huo unaifana Yanga kupanda hadi nafasi tatu ikiwa pointi 31, wakiwa nyuma kwa pointi 13 kwa vinara Simba (44) huku Azam nafasi ya pili (37).

Dar es Salaam. Bao pekee la mshambuliaji David Molinga limetosha kuipa Yanga ushindi 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Molinga alifunga bao hilo pekee katika dakika 50, akiunganisha vizuri krosi ya Ditram Nchimbi na kuihakikishia Yanga pointi tatu na kupanda hadi nafasi tatu ikiwa pointi 31, wakiwa nyuma kwa pointi 13 kwa vinara Simba (44) huku Azam nafasi ya pili (37).

Bao hilo linamfanya Molinga kufikisha mabao 6 katika orodha ya wafungaji bora inayoongozwa na Meddie Kagere wa Simba (12).

Kiwango bora alichoonyesha Molinga kiliwafanya mashabiki wa Yanga kumshangilia kwa nguvu wakati anatolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Yipke Gilman.

Molinga alipachika bao hilo dakika ya 50 akipokea pasi safi ya Nchimbi aliyeingia dakika ya 46 kuchukua nafasi ya Patrick Sibomana.

Baada ya bao hilo, Molinga alionekana kujiamini na kufanya mashambulizi kadhaa kabla ya dakika ya 67 kumchambua mchezaji wa Mtibwa, Awadh Juma na kutoa pasi ambayo hata hivyo ilichezwa na mabeki wa Mtibwa huku mashabiki wa Yanga wakimshangilia kwa nguvu.

Mtibwa Sugar walifanikiwa kumtuliza winga wa Yanga, Benard Morrison kutokana na kucheza mpira wa nguvu dhidi ya Mghana huyo.

Kiungo Mtibwa Sugar, Humud alisema alimtazama Morrison katika michezo iliyopita hivyo alijua namna sahihi ya kukabili.

“Morrison ni mchezaji mzuri kwa hiyo unapotaka kumkaba ni hakikisha hapati muda wa kukaa na mpira, ukifika unafika wewe kwa haraka, lakini sikuwa na lengo la kumchezea vibaya.

Mabadiliko yaliyofanywa na benchi la ufundi la Yanga ya kutolewa kwa Patrick Sibomana na kuingia Nchimbi yamezaa matunda katika mchezo.

Nchimbi ndiye aliyetengeneza bao la Yanga lililofungwa dakika ya 50 baada ya kupokea pasi ya Haruna Niyonzima, mshambuliaji huyo wa zamani wa Polisi Tanzania, alilazimisha na kuingia katika lango la Mtibwa na kumpasia Molinga aliyepachika bao hilo.

Hesabu za Nchimbi na Molinga ziliendana kwani wakati pasi hiyo ikipigwa alikuwa katika eneo zuri, alichokifanya ni kuumalizia mpira ule na kuwaacha mabeki wa Mtibwa Sugar na kipa wao Kado wakibebeshana lawama.

Hata hivyo dakika ya 69, Yanga ilifanya mabadiliko mengine ambapo alitolewa mfungaji wao wa bao la kwanza, Molinga na kuingia Yikpe Gnamien.

Licha ya kutolewa kwa Molinga, Yanga iliendelea kuwa  na nguvu kwenye safu yao ya ushambuliaji huku katika kipindi hicho wakionekana viungo wao wachezeshaji kutengeneza zaidi nafasi.

Kuanzia dakika ya 70, Mtibwa Sugar ambao walionekana kufunga njia za Yanga kipindi cha kwanza, walionekana kufunguka na kuanza kushambuliana kwa zamu.

Mtibwa Sugar, walifanya mabadiliko kadhaa, lakini hayakuweza kuwasaidia kupata bao la kusawazisha licha ya kutengeneza mshambulizi mfululizo katika lango la Yanga.

Kilichoonekana kuwaangusha Mtibwa Sugar katika mchezo wa leo dhidi ya Yanga ni kuingia na mbinu za kujilinda kuanzia kipindi cha kwanza hadi mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Mbinu hiyo, iliifanya Yanga kufika mara nyingi zaidi katika eneo lao kabla na wao kuzinduka na kufunguka baada ya kuruhusu bao hilo ambalo limemfanya Luc Eymael kuoata ushindi wa tatu mfululizo akiwa na kikosi hicho.

Mwamuzi asimamisha mechi kulionya benchi la ufundi Yanga

Mwamuzi wa mechi ya Yanga na Mtibwa, Emmanuel Mwandembwa amelazimika kusimamisha mechi hiyo kwa sekunde kadhaa na kwenda kutoa onyo kwenye benchi la ufundi la Yanga.

Tukio hilo limetokea dakika ya 18 ya mchezo huo unaoendelea kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam baada ya mwamuzi huyo kuamuru mpira wa kurushwa ambao Yanga waliamini ulitolewa na mchezaji wa Mtibwa urushwe kwenda kwenye lango la Yanga.

Kabla ya uamuzi huo, refarii alimuangalia mshika kibendera ambaye hakuonyesha chochote hadi refarii alipoamuru mpira huo ambao ulitoka jirani na alipokuwa anesinama kocha ya Yanga, Luc Eymael kurushwa kuelekea langoni mwa Yanga.

Kitendo hicho kilisababisha kocha Luc kuruka kimasai huku akiwa amenyoosha mikono juu kwa ishara ya kutokubaliana na uamuzi huo akimuelekea mwamuzi wa akiba huku mashabiki wa Yanga wakuzomea.

Akizungumzia mchezo huo Kocha Zuber Katwila wa Mtibwa amesema wachezaji walifuata maelekezo ndiyo sababu hawakufungwa mabao mengi.
"Kufungwa halikuwa lengo letu lakini ni hali ya mchezo, Wachezaji walifuata maelekezo, Mechi ilikuwa fifty fifty, tulianza kwa kuchezesha viungo wengi kama Yanga, lakini wao baadae wakabadilika na mbinu yao imewapa bao.
Kocha wa Yanga, Luc Eymael amesema walikosa mabao mengi na kuna nafasi za wazi za wacgezaji  wake hasa Sibomana zilikuwa wazi lakini hawakuzitumia.
"Tunafurahi tumepata pointi, pia tumepoteza nafasi nyingi za wazi," alisema Luc.

Katika michezo mingine Mbeya City imelazimishwa sare 1-1 na Azam, JKT Tanzania ilifungwa bao 1-0 Polisi Tanzania, wakati Tanzania Prison ikishinda 1-0 dhidi ya KMC.