Mkwasa analeta jembe moja tu

Saturday November 16 2019

mashabiki - Yanga-kocha-charles-Mkwasa-wachezaji-Jangwani-Yanga SC-kikosi-Mwanasport-MwanaspotiGazeti-MwanaspotiSoka-

 

By Thobias Sebastian

KAMA kuna kitu mashabiki wa Yanga wanataka kukisikia kutoka kwa mabosi wao, basi ni kuhusu wachezaji wapya ambao watatua kuongeza mzuka baada ya kuanza kwa kusuasua.

Sasa jana Ijumaa Kocha wa Muda, Charles Boniface Mkwasa (Master) amedokeza kidogo kuhusiana na mchezaji wa gani anayetarajiwa kumnasa kwenye dirisha dogo la usajili ili kuifanya Yanga kuwa tishio.

Kabla ya kuzungumza hilo, Mkwasa aliwaongoza wachezaji kwenye mazoezi yaliyofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, na baadaye akazungumza na Mwanaspoti na kueleza mipango yake ni kumshusha straika matata wa kupachika mabao.

Amesema tatizo ambalo linaisumbua Yanga kwa sasa ni ubutu wa eneo la ushambuliaji na ameuomba uongozi kumleta mtu anayejua kufunga na hapo mashabiki watafurahi na roho zao.

Hata hivyo, Mkwasa alisema siyo kama kwenye kikosi chake kwa sasa hakuna washambuliaji wazuri, wapo wengi lakini anakosekana mtu mwenye uwezo wa kukaa kwenye njia za mipira ya hatari na anayejua kuifanya vyema kazi yake ya kufunga.

“Ukiangalia timu ina washambuliaji wazuri lakini tunamkosa mtu anayeweza kufunga. Yaani mtu akipata nafasi anaitumia kwa kufunga…sio yule anayepata nafasi tano kisha anafunga moja. Tunatengeneza nafasi nyingi hata mazoezini na washambuliaji wanafunga, lakini nataka iwe zaidi kwenye mechi.

Advertisement

“Nitakutana na viongozi wangu na kuwapa mapendekezo kuhusu nini cha kufanya kwenye dirisha dogo la usajili. Lakini, kubwa nataka mshambuliaji mwenye uwezo wa kufunga. Natambua wako wengi lakini, ni suala la kukubaliana ni nani tutamchukua iwe kutoka hapa ndani ama nje ya nchi lakini hadi tukubaliane na uongozi,” alisema Mkwasa.

Katika hatua nyingine Mkwasa aliongeza katika kipindi hiki cha kusimama kwa ligi watatafuta mchezo mmoja wa kirafiki ili kuona vile ambavyo wanavifanyia kazi katika mazoezi yao ya kila siku.

“Bado tunatafuta timu ya kucheza nayo mechi ya kirafiki na nimeomba iwe siku ya Jumapili ili kuona wachezaji wamefanyia kazi kiasi gani mbinu na aina mbalimbali ya mazoezi ambayo tumekuwa tukifanya wakati huu.

“Hatutawatumia wachezaji vijana ambao, hawapati nafasi ya kucheza mara kwa mara, bali tutatumia wachezaji wale wa kikosi cha kwanza ili kuwapa hali ya kushindana na kuyafanyia kazi mapungufu ingawa mabadiliko yatafanyika,” alisema Mkwasa.

KUISUIKA YANGA MPYA

Kikosi cha Yanga jana licha ya kufanya mazoezi mbalimbali lakini muda mwingi kilifanya yale ya kucheza na Mkwasa alionekana kuchagua wachezaji wanaopata nafasi katika kikosi cha kwanza kufanyia kazi mazoezi hayo.

Ilikuwa hivi, Mkwasa aliwaweka katika timu moja kipa Farouk Shikalo, Juma Abdul, Jaffary Mohammed, Ali Ali, Ally Sonso, Kabamba Tshishimbi, Mo Banka, Mapinduzi Balama, David Molinga, Sadney Urikhob na Mrisho Ngassa.

Baada ya kuwagawa Mkwasa alitaka mpira uanzie kwa Shikalo ambaye atampasia Ally ambaye naye atampasia beki wa pembeni Abdul akiwa anakimbia pembeni huku mpira ukiwa amempasia kiungo wa kati Balama, ambaye naye atapiga pasi tena kwa Abdul muda huo akiwa katika eneo la timu pinzani atapiga krosi au pasi ya chinichini kwa washambuliaji Molinga na Sadney ambao, jukumu lao lilikuwa kufunga tu.

Mkwasa alisema wakati anaingia katika timu aliona wanashindwa kuandaa mashambulizi yao kutoka nyuma na aina ya kushambulia ndio maana wameamua kufanya zoezi hilo ambalo limeanza kuzaa matunda.

“Katika mpira ukiondoa ile kuanza katikati mkiwa mmefunga ua kuanza wakati wa mechi au mapumziko muda wote lazima muanzie kucheza kutokea nyuma sasa hilo ndio nimeanza kulijenga katika kikosi changu,” alisema.

“Tutakuwa na uwezo mkubwa wa kujenga na kuanza mashambuliazi kutokea nyuma ambayo kama tukiweza kulifanya hili zoezi vizuri hilo litatusaidia kushambulia muda mwingi na kumiliki mpira kwani wakati nikiwa sijaanza majukumu haya nimekuwa nikizifutilia timu za Ligi Kuu na kubaini mapungufu yao,” alisema Mkwasa ambaye amewahakikishia mashabiki timu hiyo itakuwa vizuri na kuanza kupachika mabao.

Advertisement