Mkongo aipiga chenga Yanga

MASHABIKI wa Yanga kwa wiki nzima wamekuwa na mzuka wakiamini kuna mashine mbili za Simba zilikuwa njiani kutua Jangwani, akiwamo winga Deo Kanda na kiungo fundi wa mpira, Clatous Chama.

Hata hivyo, ndoto za Yanga kumnasa Mkongoman, Deo Kanda zimeyeyuka baada ya winga huyo aliyeifungia Simba mabao manane msimu huu, kuwakatili Jangwani kwa kusaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kuitumikia timu hiyo.

Licha ya Simba kumsainisha mkataba huo, lakini huenda mambo yanaweza kuwa magumu kusalia Msimbazi, kutokana na wamiliki wa winga huyo, TP Mazembe kudaiwa wanataka mkwanja mnene.

Iko hivi. Uongozi wa Simba ulimuita Kanda mezani kuzungumzia masuala ya mkataba wake mpya baada ya ule wa awali wa miezi sita kuelekea ukingoni mwisho wa msimu huu na katika mazungumzo hayo Simba iliwakilishwa na aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wao, Senzo Mazingisa.

Katika mazungumzo hayo upande wa Kanda uliafikiana na Simba kupatiwa Dola za Kimarekani 50,000 zaidi ya (Sh 100 milioni) na kusaini mkataba mpya wa miaka miwili.

Mwanaspoti ilipata taarifa kutoka ndani ya Simba, iliyoeleza baada ya makubaliano hayo kabla ya kumwekea pesa Kanda, katika akaunti yake, mabosi wa Mazembe waliwambia Simba na wao wanataka Dola 50,000 ili waweze kumuachia moja kwa moja winga huyo.

“Hatuwezi kutoa Dola 100,000 (zaidi ya Sh230 milioni), ili kummiliki Kanda moja kwa moja na si kuwa naye kwa miaka miwili kwa mkopo kama ilivyokuwa hapo awali kama ambavyo Mazembe wanataka kwani tuna wachezaji wengi ambao wanacheza katika eneo lake,” chanzo kilisema.

“Kweli tunamhitaji Kanda lakini pesa ambayo tulitaka kumpa baada ya kuongezwa na Mazembe ni nyingi mno ambayo hatupo tayari kuitoa kwa maana hiyo kama watakubali ambayo tunayo tutamchukua lakini wakikataa tutamuachia,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Unajua kuna kiungo Jean Vital Ourega kutokea Mazembe tupo katika mipango naye kwa maana hiyo lazima twende sawa na wenzetu hawa ili tukubaliane katika masuala yote mawili haya.”

Kanda alipotafutwa na Mwanaspoti alithibitisha kuwa ni kweli alishamalizana na Simba na kusaini mkataba mpya wa miaka miwili ambao utamalizika mwisho wa msimu wa 2021-22.

“Niliongeza mkataba mpya na Simba wa miaka miwili baada ya ule wa awali wa miezi sita kuelekea mwisho, wakati ligi ikiwa imesimama kutokana na janga la corona na muda ukifika watalieleza hilo, lakini taarifa za kwenda timu nyingine iliyokuwa ndani ya nchi hii hilo halipo,” alifafanua Kanda.

MSIKIE KASHASHA

Mchambuzi wa masuala ya soka nchini, Alex Kashasha alisema Simba wanakwenda kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa kwa maana hiyo wanahitaji kuwa na wachezaji wenye ubora wa kucheza mashindano hayo makubwa Afrika kwa ngazi ya klabu.

“Simba wanahitaji kuwa na wachezaji wazoefu na wakomavu katika kikosi chao kama Kanda, ndio wataweza kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo kama hauna timu nzuri huwezi kufikia malengo yao,” alisema.