Miujiza Taifa kati ya Simba na Yanga Jumapili

Friday July 10 2020

 

By CLEZENCIA TRYPHONE

KAMA rekodi zitaongea au kujirudia Simba huenda wakamaliza mechi dhidi ya Yanga, Jumapili hii kirahisi sana, lakini mastaa wa zamani wamesema mechi hiyo itakuwa tofauti kabisa.

Timu hizo zinakutana kwenye mechi ngumu ya nusu fainali ya Kombe la FA ambalo litaamua mambo mawili muhimu. Mechi hiyo itaamua Simba isonge fainali kubeba kombe la pili au Yanga ifuzu fainali kusaka tiketi pekee ya kucheza kimataifa msimu ujao ama imalize msimu kinyonge.

Katika kuonyesha presha ya mchezo huo ilivyo juu, Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck jana baada ya timu yake kutua Dar es Salaam ikitokea Lindi ilikopewa kombe lao alikataa wachezaji wasitembee mitaani wakishangilia ubingwa na mashabiki.

Lakini Kocha wa Yanga, Luc Eymael ameibakiza timu yake kambini mjini Bukoba kujiandaa na mchezo huo ambao amesisitiza utakuwa na nafasi kubwa ya kuamua ubora wa kikosi hicho msimu ujao.

Rekodi zina sehemu yake kwenye mchezo wa soka duniani kote ingawa katika miaka ya hivi karibuni zimekuwa zikivunjika.

Lakini tangu chama tawala (CCM) kianzishwe mwaka 1977, mwanamieleka John Cena na mwanamuziki Kanye West wazaliwe, Simba imekuwa na rekodi za kutisha inapokutana na Yanga mwezi huu wa Julai. Rekodi zinaonyesha tangu mwaka 1977 ambayo ni miaka 43 iliyopita, Simba na Yanga zimekutana kwenye mashindano mbalimbali ndani ya mwezi Julai mara 10.

Advertisement

Katika mara hizo, Simba imeshinda michezo saba, sare mbili na kupoteza mechi moja ambazo ni sawa na pointi 23. Ni rekodi za kibabe ambazo zinawapa jeuri Simba ingawa Yanga na wameonekana kupuuzia.

Yanga katika rekodi hizo za mwezi Julai tangu enzi hizo imeshinda mchezo mmoja tu, sare mbili na kuambulia pointi tano.

Lakini hata hivyo kwenye rekodi za jumla kwenye Ligi Kuu Bara pekee tangu 1965, timu hizo zimekutana mechi 104, Yanga imeshinda 37, Simba 31 lakini Simba imepoteza michezo 37 huku Yanga ikipoteza 31.

ISHU YA REKODI

Licha ya rekodi hizo, wachezaji wawili wa zamani wa klabu hizo, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ na Ally Mayay Tembele wamesisitiza kuwa mechi hiyo haina mwenyewe.

Mayay alisema kwa tathmini ya kawaida Simba ni bora kuliko Yanga, hivyo ikiingia uwanjani na mawazo hayo mchezo unaweza kuwa mgumu kwa upande wao.

“Timu hizi zinapokutana huwa kuna matukio yanayozua mijadala mingi - mfano hizo historia, zina faida na hasara hasa kwa wale ambao wanafanya, wanataka kuvunja rekodi kwani katika mchezo huu saikolojia nayo huwa inaamua matokeo katika mchezo husika.

“Mechi inayowakutanisha hawa jamaa wawili inakuwa na mambo mengi lakini pia mipango ya mwalimu husika inaweza kuamua matokeo siku hiyo kwa upande wowote ule, tumeona licha ya ubora wa Simba lakini mechi ya raundi ya kwanza ilitoka sare na raundi ya pili ikafungwa,” alisisitiza na kuongeza kuwa hata sekunde moja inatosha sana kuamua mchezo huo na rekodi zikatupiliwa mbali.

kwa upande wake, Mmachinga alisema mchezo huo hauna cha historia wala nini kwa kuwa hautabiriki.

Alisistiza kuwa anatarajia kuona mpira mzuri na wenye burudani kutokana na kila timu kuhitaji matokeo.

“Unaweza ukawa bora na ukafungika, na usiwe bora ukafunga ni Mungu tu na dakika 90 zitaamua, ila kimtazamo wengi wanaipa Simba nafasi kutokana na ubora wao lakini mpira haueleweki hasa wanapokutana hawa,” alisema mchezaji huyo wa zamani.

Advertisement