Mgosi atabiri mazito Simba

Muktasari:

Moja ya michezo ambayo alisema hataisahau maishani mwake akiwa na kikosi cha Simba ni pale walipoivua ubingwa wa Afrika Zamalek mwaka 2003.


NAHODHA wa zamani wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’ amesema ili timu hiyo iweze kufika mbali kimataifa msimu huu, ni lazima ianze vyema ugenini hapo kesho Jumamosi dhidi ya UD Songo.

Alisema tatizo kubwa la Simba msimu uliopita lilikuwa ni kupata matokeo mabaya ugenini na ilipofika nyumbani ilivuna matokeo mazuri, hivyo ana imani msimu huu kocha na uongozi utakuwa umelitazama hilo.

“Naamini Simba imeonja utamu wa mashindano haya, hivyo wachezaji wanapaswa kujitambua, viongozi na makocha wafanye kazi zao ili mwisho wa siku wahakikishe wanapata matokeo yatakayowabeba katika mchezo wa marudiano,” alisema Mgosi.

Aliongeza katika usajili uliofanywa umeonyesha kiasi gani kikosi kilivyo kizuri, hivyo kila mchezaji anapaswa kuonyesha ubora kwenye eneo lake na kutobweteka kwa sifa za mashabiki.

Mgosi alisema siku zote kwenye soka huwa hawangalii kukosekana kwa mtu mmoja kama wengi walivyoanza kujadili kutokuwepo kwa Emmanuel Okwi msimu huu. Okwi amesajiliwa na Al-Itihhad ya Misri.

“Kila mchezaji ni bora kwenye nafasi yake kwani atakayekuwepo atafanya vizuri na hata kama Okwi angekuwepo kwa sababu kila mmoja ana umuhimu wake.”

Moja ya michezo ambayo alisema hataisahau maishani mwake akiwa na kikosi cha Simba ni pale walipoivua ubingwa wa Afrika Zamalek mwaka 2003.

Simba ilishinda bao 1-0 nyumbani kisha kufungwa bao 1-0 ugenini na kwenda kwenye mikwaju ya penalti huku tuta la mwisho likifungwa na Christopher Alex (marehemu) lililoibeba Simba.