Mayanja huko KMC, acha kabisa

Monday July 15 2019

 

By Doris Maliyaga

WENYE misemo yao huwa wanasema bahati ya mtende, vile ambavyo anakutana nayo, Kocha wa KMC, Jackson Mayanja ‘Mia Mia’ kwenye soka la Tanzania.

Licha ya kutokea Uganda ambako amezaliwa na kuchezea kwa kiwango kikubwa timu ya taifa ‘The Cranes’, hii sasa ni mara ya nne kuitwa kuzinoa klabu za Ligi Kuu Bara.

Mayanja ambaye pia ameifundisha timu ya Taifa ya Uganda miaka ya nyuma. Akiwa Tanzania alikuwa kocha msaidizi wa Simba akimsaidia, Muingereza Dylan Kerr na baadaye Mcameroon Joseph Omog na msimu wa 2017-2018, aliamua kurudi kwao kwa mapumzika.

Hata hivyo, kabla ya Simba, Mayanja alizifundisha Kagera Sugar pamoja na Coastal Union na sasa KMC timu zinazokamilisha idadi hiyo nne kwa timu za Tanzania.

Mkataba wake mpya na KMC ni kuifundisha kwa kipindi cha mwaka mmoja akichukua mikoba ya Mrundi Etienne Ndaiyagije aliyejiunga na Azam FC na sasa amepewa majukumu ya kuinoa timu ya Taifa Stars inayojiandaa na CHAN.

Uwepo wake KMC lazima afanye kazi ya maana maana Ndaiyagije ameifanyia makubwa sambamba na kuwapa nafasi ya kuiwakilisha Tanzania Kombe la Shirikisho Afrika.

Advertisement

APEWA GARI, NYUMBA YA KISASA

Kocha huyo alipofika Dar es Salaam, KMC walimpangia moja ya hoteli kubwa Dar es Salaam, lakini sasa amepangiwa nyumba kubwa na ya kisasa maeneo ya Makongo jijini Dar es Salaam.

“Niliambiwa nichague kati ya kukaa hotelini au nipangiwe nyumba, nimechagua nyumba. Nimefanya hivi kwa ajili ya kuishi pamoja na familia yangu mke na watoto wangu huwa wanakuja mara kwa mara,” anasema Mayanja.

Achana na nyumba, ukiwa mtaani jijini Dar es Salaam gari ya kutembelea ndio mpango mzima, KMC imempa Mayanja gari ya kisasa aina ya Kluger yenye rangi ya silva na anaendeshwa na dereva kwa raha zake: “Gari vitu vya kawaida kabisa ni maisha tu.”

ANAVYOIONA KMC NA MIPANGO YAKE

“Lengo ni kufanya timu kuwa kubwa na ushindani. Kwa nilivyoona hadi nikakubali kufanya kazi na KMC ni baada ya kuona mpango kazi wao, wana malengo na watekelezaji,” anasema Mayanja ambaye mkataba wake ni wa mwaka mmoja.

“Kwa sasa nataka kutengeneza KMC icheze mchezo wa kuvutia na kuwa mfano kwenye ligi hii na kitu kizuri, napata sapoti kubwa kutoka kwa Meya wa Manispaa ya Kinondoni (Benjamini Sitta).” Anasema kwa sababu timu hii pia ni Manispaa kuwafanya wenyeji na watu wengine kuishabikia KMC kama zilivyo timu za England na akaitolea mfano Liverpool.

“Uongozi, wachezaji na mashabiki wanatakiwa kuacha kufikiria karibu ili kuona timu inapata mafanikio.”

USAJILI, WACHEZAJI VIJANA

Mayanja ambaye ameingia KMC na kukuta sehemu kubwa ya usajili umefanywa, lakini akasisitiza jambo hilo si tatizo kwake.

“Wachezaji wa Tanzania sehemu kubwa ya viwango vyao vinafanana, ni wachache ambao huwa na upekee. Nilionao kwenye timu wengi vijana wana nidhamu na tunafanya kazi vizuri tangu nimefika,” anasema Mayanja.

Amesema huo ni mwanzo mzuri kwa timu hasa katika suala zima la nidhamu na mambo mengine katika kuona wanafikia malengo.

WALIVYOJIPANGA SHIRIKISHO

Kwa mara ya kwanza KMC inashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa chini ya Kocha Mayanja anasema wanakwenda kufanya majabu kama maandalizi yao yatatosheleza.

“Mashindano hayo ni makubwa yanataka maandalizi ya hali ya juu tofauti na ilivyo kwenye ligi lakini ninachopenda kuwaambia mashabiki wa soka KMC itafanya vizuri na kuweka historia kwa kufanya vizuri,” anasema Mayanja.

Anasema, pamoja na mandalizi mengine wanayofanya Kagame itawapa picha kamili ya kufahamu ubora wao kimataifa.

BOKUNGU, MIGI KAZI MAALUMU

Kocha Mayanja amebainisha mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika yanahitaji zaidi wachezaji wenye uzoefu na ndio maana akawasajili, Mkongo Besala Bukungu na Mugiraneza Jean Baptist ‘Migi’.

“Kutokana na aina ya wachezaji ambao ninao kikosini wengi ni vijana wadogo wanaweza kufanya vizuri kwenye ligi lakini mashindano ya Afrika wakashindwa na kinachosababisha ni uzoefu,” anasema Mayanja.

“Ndio maana usajili wa Bukungu na Mugiraneza utakuwa muhimu zaidi katika mashindano kama haya, lakini bado kuna wazoefu wengine kama kipa wetu Juma Kaseja wakichanganyika na hawa wengine mambo yatakuwa mazuri.”

MTOGO AMTOA KAULI

Mbali na Bokungu, Migi mpaka sasa kikosi cha KMC kina wachezaji watatu kutoka nje ya nchi pamoja na Mtogo Serge Alannogue ambaye ni kijana mdogo ana miaka 18 kutoka klabu ya Glory.

“Mtogo ni mchezaji mzuri, kijana mdogo lakini ana kitu kikuwa hata ukiwa naye kwenye timu una kitu. Lakini, bado naendelea kumwangalia zaidi katika mechi mbalimbali,” anasema Mayanja.

TOFAUTI YA SIMBA NA KMC

Mayanja anasema, ipo tofauti kubwa kati ya Simba aliyoifundisha miaka ya nyuma na KMC anayoifundisha sasa kutokana na mambo mbalimbali.

“Simba ni timu nzuri sawa na KMC lakini kuna tofauti kubwa. Simba ni timu kubwa, wakongwe na tayari wameshajikusanyia mashabiki wengi, kufikia huko ni prosesi,” anasema Mayanja.

Anasema hataki kuifananisha KMC na Simba au Yanga kwa sababu ni vitu viwili tofauti.

“Ukizungumzia Ligi ya Tanzania Simba na Yanga ziko miaka na miaka. Zimeshajitengenezea mashabiki wake na wana nguvu. Mimi sitaki kushindana na Simba au Yanga kwa sababu kazi niliyonayo ni kutengeneza timu yangu ifanye vile ninavyotaka pamoja na waajiri wangu,” anasema Mayanja.

Anasema hata KMC itakuwa na mashabiki wengi tu na watafata ubora wa kiwango.

KINACHOIUMIZA TAIFA STARS

Mayanja anasema tatizo kubwa linaloiumiza timu ya Taifa Stars ni mipango na kitu kikubwa ambacho wamekipatia kwenye kikosi chao cha Uganda ‘The Cranes’ ni hiki.

“Kikosi ambacho unakiona sasa hivi Uganda kilichoshiriki AFCON sehemu kubwa ya wachezaji nilikuwa nao 2010, wakati naifundisha timu hiyo.

“Tuliwatengena na kuwajenga kwenye timu tangu wakiwa wadogo na ndio sasa wanaofanya vizuri kwenye timu,” anasema Mayanja ambaye sehemu ya wachezaji hao ni kipa Denis Onyango anayekipiga Mamelodi Sandowns ya Afrika na mshambuliaji wa zamani wa Simba, Emmanuel Okwi, Hassan Waswa na Wadada.

Amesema, mbali na hiyo miapango ya kikosi hicho cha taifa: “Ukienda Uganda kuna wachezaji wengi wa timu ya taifa kwa sababu tumegawa kila wachezaji wana majukumu yao.”

“Timu ya taifa ina vikosi vitatu, cha AFCON, CHAN na U-23 ukiachana na zile nyingine za vijana kama U-17 na U-15. AFCON ni upana kutoka mataifa tofauti, CHAN ni wale wa ndani sasa kwa Tanzania hakuna mgawanyo mzuri wa vikosi hivyo,” anafafanua Mayanja.

Amesema, hapa Taifa Stars inamwangalia Mbwana Samatta anayekipiga Genk ya Ubelgiji na Simon Msuva wa Jadida na wasipokuwepo kila kitu kinaharibika.

ABDI BANDA, KICHUYA WAMPA RAHA

Mayanja anasema, alikuwa miongoni mwa jopo la makocha lililopendekeza usajili na kufanya kazi pamoja na wachezaji hao alipokuwa anaifundisha Simba, lakini kwa sasa wanafanya vizuri kimataifa.

“Kichuya alikuwa Morogoro huko (Mtibwa Sugar), lakini baada ya kusajiliwa na Simba alifanya vizuri na kupata timu nje ya nchi sawa na ilivyo kwa Abdi Banda ambaye kwa sasa anacheza Baroka FC ya Afrika Kusini alitokea Tanga Klabu ya Coastal,” alisema Mayanja na Kichuya aliyemtaja kwa sasa anacheza Petrojet ya Misri.

ANA SIRI NA MO IBRAHIM

Bila shaka kutua kwa Mohammed Ibrahim ‘Mo Ibrahim’ ndani ya kikosi cha KMC akitokea Simba iliyomtoa kwa mkopo ni maombi ya Mayanja ambaye anaweka wazi ni mchezaji ambaye anapenda kufanya naye kazi.

“Wapo wachezaji wengi lakini binafsi kwangu, Mo Ibrahim ni mchezaji mzuri na ninachoamini atanifanyia kazi nzuri kwenye timu. Huwa najiuliza kwa nini hapati nafasi ya kucheza, nafikiri wakati tupo naye Simba alikuwa anapata nafasi,” anasema Mayanja.

Hata hivyo, kumekuwa na madai Mo Ibrahim amekuwa na tatizo kwenye nidhamu jambo ambalo Mayanja amelielezea ni namna wanavyoishi.

“Suala la nidhamu ni muhimu kwenye timu lakini ni mchezaji husika na wewe mwenyewe namna mnavyoishi,” anasema Mayanja.

KUFANYA KAZI NA KABANDE

Baada ya kumaliza na KMC tu, kocha wake msaidizi akawa, Mrage Kabange ambaye amefanya naye kazi kwenye timu tofauti kama Kagera Sugar na Coastal Union.

“Kufanya kazi na Kabange ni kwa sababu anajua filosofi yangu. Nimefanya kazi na Kabange kwa kipindi kirefu hata kuacha maagizo kwake linakuwa rahisi kwa sababu unajua kila kitu kitakwenda sawa,” anasema Mayanja.

FILOSOFI YA MAYANJA NI HII

Mayanja ambaye wakati anaifundisha Kagera Sugar alikuwa maarufu kwa jina la Marashi staili. Hii ni kutokana na yeye mwenyewe kusema aina ya soka analofundisha ni Marashi staili.

“Napenda kucheza mpira wa kushambulia zaidi, nguvu na akili mwenyewe napenda kuita Marashi staili, hili ndio soka ninalolihitaji zaidi sasa Kabange anaijua vizuri,”anasema Kabange.

Anasema, anaamini Kabange ni kocha mkubwa Tanzania lakini ndio hivyo mara chache amekuwa ana timu.

AWAZUNGUMZIA OMOG, KERR

Alipokuwa kocha msaidizi Simba, Mayanja alifanya kazi na makocha Muingereza Dylan Kerr na Mcameroon Joseph Omog katika nyakati tofauti, anawazungumzia.

“Nilifanya nao kazi vizuri kwa kipindi chote, ni makocha wazuri kama Omog ni mzoefu na Kerr pia. Kila mtu ana ubora na mapungufu yake lakini kilikuwa kipindi kizuri,”anasema Mayanja.

ALIKUWA WAPI ALIPOONDOKA SIMBA

“Baada ya kuachana na Simba malengo yangu yalikuwa ni kupumzika na kuwa karibu na familia yangu. Nilipumzika kwa muda lakini baadaye kuna timu ya mtaani kwetu iliniomba niifundishe kwa sababu walikuwa na malengo ya kupanda Ligi Kuu inaitwa KFC,”anasema Mayanja.

Anasema, alikubali kwa sababu hakuwa na namna ni timu ya nyumbani na alifanikiwa kuipandisha Ligi Kuu Uganda ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu ianzishwe.

“Baada ya kuipandisha nikawa nimekamilisha ahadi na ndipo KMC wakanifata nifanye nao kazi msimu huu,”anaeza Mayanja na kufafanua KFC ipo katika mji wa Mkono njia ya kwenda Jinga.

ANAMILIKI TIMU UGANDA

Mayanja anamiliki timu ya vijana wadogo nchini Uganda inayoitwa Mia Mia Academy na ni maarufu sana Uganda. Ameweka wazi, ujio wake KMC ameiacha KFC pamoja na msaidizi wake.

“Mia Mia ni timu ina uongozi na miapango yake. Kwa sasa kuna kocha anaisimamia hivyo hata kuwepo huku hakuathiri kitu,” anasema Mayanja anayeweka wazi anapenda muziki wenye miondoko ya taratibu yoyote.

“Lengo la kuwa na timu hiyo kwa ajili ya kuendeleza vijana wadogo ambao wakiendelezwa ndio wanaokuja kufanya vizuri hapo baadaye na kusaidia timu zetu za taifa.”

ANAPENDA AFRIKA

Wakati sehemu kubwa ya Watanzania pamoja na Afrika macho yao ni kwenye soka la Ulaya lakini Mayanja anasema yeye ni mpenzi zaidi wa soka la Afrika.

“Nafuatilia zaidi mpira wa Afrika kwa sababu ndio naupenda kama AFCON ndio nafatilia zaidi na naipenda timu yangu ya Uganda. Ulaya kidogo anaifatilia Ligi ya Bundasiliga na La Liga,” anasema Mayanja na kumtaja Neymar kuwa mchezaji wake bora.

“Brazil walimwacha Neymar kwa madai ya utovu wa nidhamu lakini ndio hivyo, kwangu ni mchezaji bora.”

KIKOSI CHA KMC

KMC ambao kama wamebeba krimu ya wachezaji wazawa wanaofanya vizuri kwa sasa, imewasajili Haruna Shamte kutoka Lipuli FC, Vitalis Mayanga na Abdallah Mfuko walionaswa kutoka Ndanda FC, Six Isabilo na Amos Charles walikuwa na Stand United.

Wengine ni Ramadhani Kapera kutoka Kagera Sugar, Kenny Ally aliichezea Singida United, Aron Karambo kutoka Tanzania Prisons na Salum Aiyee wa Mwadui FC, Mo Ibrahim katoka kwa mkopo Simba, Bokungu, Migi na Serge.

Advertisement