Mayanja azitaja Simba, Kagera Sugar

Muktasari:

Jackson Mayanja kwa sasa anaifundisha timu ya Kyetume inayoshiriki Ligi Kuu ya Uganda aliyojiunga nayo mwishoni mwa mwaka jana akitokea KMC.


KOCHA Jackson Mayanja raia wa Uganda amezitaja Simba na Kagera Sugar kama timu alizofurahia zaidi kufanya nazo kazi  katika kipindi cha miaka nane (8) aliyofundisha soka nchini hapa.

Kocha huyo anayeifundisha Kyetumme ya Uganda kwa sasa, amesema kuwa alifanya kazi katika mazingira mazuri zaidi pindi alipozinoa timu hizo mbili kulinganisha na nyinginezo.

"Ukiniambia nitaje mahala ambako nilikuwa na furaha zaidi katika kazi yangu ya ukocha huko Tanzania basi ni Simba na Kagera Sugar.

"Nilikuwa na ushirikiano mkubwa na makocha wenzangu, wachezaji, viongozi na mashabiki na waliniona sehemu ya timu yao na walinipa sapoti ya hali ya juu katika kutimiza majukumu yangu.

"Coastal Union na KMC sikuwa na matatizo nao na nilifanya kazi kwa furaha lakini niwe mkweli tu kwamba Simba na Kagera Sugar ndizo timu ambazo nilikuwa na furaha zaidi," alisema Mayanja.

Kocha huyo alisema katika miaka zaidi ya nane aliyofundisha Tanzania, amegundua kuwa idadi kubwa ya wachezaji wana vipaji ingawa hawajitumi.

"Huwezi kufika mbali kisoka kama haujitumi. Nyie Tanzania mna wachezaji wazuri ila wanakabiliwa na tabia ya uvivu.

"Wakijituma na kuwa fiti, wengi watafika mbali kwani wana vipaji lakini hiyo pekee haitoshi," aliongeza Mayanja.