Mastraika waliofikisha mabao 50 Italia fasta

Thursday February 13 2020

Mastraika waliofikisha mabao 50 Italia fasta, ushindi wa Juventus,Fiorentina, Cristiano Ronaldo,Ligi Kuu Italia,

 

Turin ,Italia. KATIKA ushindi wa Juventus wa juzi kati wa mabao 3-0 dhidi ya Fiorentina, Cristiano Ronaldo alifikisha jumla ya mabao 50 kwenye Ligi Kuu Italia.

Ronaldo ametumia mechi 70 kufikisha mabao 50, kwa takwimu hizo anashika nafasi ya ngapi miongoni mwa magwiji ambao wamecheza Italia na walitumia mechi chache kufikisha mabao 50 katika historia ya Ligi hiyo.

10. GONZALO HIGUAIN (Mabao 50, Mechi 96)

Muargentina huyu kwa sasa anaweza kuwa Juventus, lakini alifunga bao lake la 50, Italia akiwa na Napoli mwaka 2015 siku ambayo timu yake iliipiga Sampdoria mabao 4-2.

Higuain alifunga bao lake hilo la 50 katika mechi ya 96 akiwa na kikosi cha Napoli. Tangu wakati huo ameendelea kuwa straika mkali akizunguka kwenye timu za Real Madrid, Chelsea, AC Milan na Juventus.

9. ADRIANO

Advertisement

(Mabao 50, Mechi 95)

Mbrazil huyu alipita katika timu za Inter Milan, Fiorentina, Parma na Kurudi tena Inter ambako ndiko alifunga bao lake la 50 ikiwa katika mechi yake ya 95.

Adriano alikuwa anatabiriwa makubwa mwanzoni mwa miaka ya 2000, lakini uzito ulikuja kumharibia maisha yake ya soka, msimu wa 2004-05 ndiyo ulikuwa bora zaidi kwake kutokana na kufunga mabao 42 akiwa na klabu na timu ya taifa.

8. EDIN DZEKO

(Mabao 50, Mechi 92)

Straika wa zamani wa Manchester City, alifunga mabao 10 katika mwaka wake wa kwanza Italia, kisha akafunga mabao 39 katika mwaka wake wa pili. Alifunga bao lake la 50 akiwa na kikosi cha Roma, Agosti 26, 2017 katika pambano dhidi ya Inter Milan.

Karibuni hapa amefunga bao lake la 100 akiwa na Roma katika mechi dhidi ya Sassuolo ni wazi kuwa sasa Dzeko ni shujaa wa klabu hiyo ya Italia.

7. DAVID TREZEGUET (Mabao 50,

Mechi 86)

Alifikia na kuvuka mabao 50 baada ya kufunga hat-trick dhidi ya Chievo Verona, Januari 19, 2003. Alistaafu soka Juventus akiw ana mabao 171 ya Serie A.

Trezeguet ni moja kati ya wachezaji bora kabisa kwenye historia ya Juventus ambayo imewahi kuwa na wachezaji kama Roberto Baggio, Zinedine Zidane, Michel Platini na Alessandro Del Piero.

6. GABRIEL BATISTUTA

(Mabao 50, Mechi 85)

Alifunga mabao 50 akiwa na Fiorentina – na alifanya hivyo kwa kuvunja rekodi ya Serie A, alianza msimu wa 1994-95 kwa kufunga mabao kwenye mechi 11 mfululizo akivunja rekodi ya straika wa Bologna, Ezio Pascutti (aliyefunga kwenye mechi 10 mfululizo mwaka 1962).

5. MICHEL PLATINI (Mabao 50, Mechi 84)

Mchezaji huyu wa kimataifa wa Ufaransa alifunga bao lake la 50 katika msimu wake wa pili akiwa na Juventus alifanya hivyo baada ya kufunga mabao mawili katika mchezo dhidi ya Torino, Februari 26, 1984.

4. MARCO VAN BASTEN (Mabao 50, Mechi 83)

Alihitaji misimu mitatu kufunga mabao 50, straika huyu wa Kiholanzi alifanya hivyo kwa kufunga kwa penalti katika mchezo dhidi ya Cesana on Januari 7, 1990. Aliondoka Italia akiwa na mabao 125.

Japokuwa alianza taratibu, lakini aliondoka akiwa staa na shujaa wa timu, huku akishinda tuzo ya Ballon d’Or msimu wa 1988-89 na alitwaa kiatu cha dhahabu katika msimu wa 1989-90 na 1990-91 anatajwa kama mchezaji bora wa muda wote wa AC Milan.

3. RONALDO DE LIMA

(Mabao 50, Mechi 77)

Kabla ya Cristiano, kulikuwa na R9. Mbrazil ambaye alizitesa sana beki za timu pinzani na alihitaji mechi 77 tu kufikisha mabao 50, hii ilikuwa katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Piacenza, Oktoba 2, 1999 akiwa na kikosi cha Inter Milan.

Inter Milan walimsajili kwa ada ya rekodi ya dunia kwa Pauni 13.2 milioni kutokea Barcelona mwaka 1997, miezi michache baada ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kuchukua tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia wa Mwaka.

2. CRISTIANO RONALDO (MABAO 50, MECHI 70)

Baada ya kutua Juventus msimu uliopita alifunga mabao 28, alifikisha bao la 50 katika pambano dhidi ya Fiorentina, straika huyo kwa sasa amefunga kwenye mechi 10 mfululizo za Serie A.

1. ANDRIY SHEVCHENKO

(MABAO 50, MECHI 69)

Gwiji huyu wa AC Milan ndiyo mchezaji pekee ambaye alihitaji mechi chache zaidi kufikisha mabao 50, alihitaji mechi 69 tu.

Katika msimu wake wa kwanza alifunga mabao 29, kisha akifikisha mabao 50 katika msimu wake wa pili, katika mechi ambayo timu yake ilishinda kwa mabao 3-2 dhidi ya Roma Januari 21, 2001.

Advertisement