Mastaa wakubwa wa Afcon 2019 waliozaliwa Ulaya

Friday July 12 2019

 

CAIRO, MISRI.WAKATI fainali za Mataifa ya Afrika zikiendelea pale Misri, ikumbukwe kwamba kuna mastaa wakubwa wa bara la Afrika waliozaliwa Ulaya lakini waliamua kuchezea timu zao za awali kutoka kwa mataifa ambayo wazazi wao walitoka au kuzaliwa. Wafuatao ni baadhi ya mastaa hao.

Nicolas Pepe (Ivory Coast, kazaliwa Ufaransa)

Winga wa kushoto wa Ivory Coast ambaye ameiongoza nchi hiyo kufika hatua ya robo fainali ingawa mpaka sasa nyota yake haijawaka vema. Pepe alizaliwa Ufaransa Magharibi mwa jiji la Paris miaka 24 iliyopita huku wazazi wake wakiwa na asili ya Ivory Coast.

Aliichezea Ivory Coast mechi ya kwanza dhidi ya taifa alilozaliwa Ufaransa mwaka 2016. Kwa kiwango chake cha sasa angeweza kucheza timu ya taifa ya Ufaransa.

Hakim Ziyech (Morocco, kazaliwa Uholanzi)

Kiungo mchezeshaji wa Morocco ambaye alitamba katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu ulioisha akiwa na kikosi cha Ajax ambacho alikifikisha nusu fainali ya michuano hiyo kabla ya kutolewa na Tottenham. Ziyech ambaye alikosa penalti muhimu katika pambano dhidi ya Benin alizaliwa katika mji wa Dronten nchini Uholanzi huku baba yake akiwa anatoka Morocco.

Advertisement

Staa wa zamani wa Uholanzi, Marco Van Basten ambaye alikuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Uholanzi wakati Ziyech akichagua kuichezea Morocco alikasirishwa na uamuzi huo huku akihoji kwa hasira: “Unawezaje kuwa mpumbavu kuchagua kuichezea Morocco wakati unakaribia kuitwa timu ya taifa ya Uholanzi?” Wakati huo Ziyech alikuwa amezichezea timu za Uholanzi chini ya miaka 19, 20 na 21. Mpaka sasa ameichezea Morocco mechi 21 na kufunga mabao 12.

Kalidou Koulibaly (Senegal, kazaliwa Ufaransa)

Mlinzi wa kati wa Senegal ambaye ni nguzo ya timu hiyo. Koulibaly ambaye kwa sasa anawindwa na klabu kubwa za Ulaya kwa dau la zaidi ya Pauni 80 milioni, alizaliwa katika jiji la Paris nchini Ufaransa na pia aliwahi kuiwakilisha Ufaransa katika michuano ya Kombe la Dunia chini ya umri wa miaka 20 mwaka 2011. Hata hivyo, aliamua kucheza katika taifa la wazazi wake Senegal Septemba 2015 na tangu hapo ameichezea Senegal mechi 35.

Harry Veldwijk (Afrika Kusini, kazaliwa Uholanzi)

Kama ilivyo kwa Ziyech wa Morocco, Veldwijk pia alizaliwa nchini Uholanzi katika mji wa Uithoorn kaskazini mwa nchi ya Uholanzi. Alicheza mechi yake ya kwanza kwa timu ya taifa ya Afrika Kusini Oktoba 2016 katika pambano dhidi ya Msumbiji ambalo lilimalizika kwa sare ya 1-1.

Hata hivyo, ilimchukua mshambuliaji huyu wa Sparta Rotterdam miaka miwili na nusu kucheza mechi nyingine ya Afrika Kusini dhidi ya Libya Machi mwaka huu.

Riyad Mahrez (Algeria, kazaliwa Ufaransa)

Mmoja kati ya mastaa wakubwa katika soka la Afrika na England. Staa huyu wa Manchester City angeweza kuwa mchezaji wa timu ya taifa ya Ufaransa, lakini badala yake alichagua kucheza katika kikosi cha Algeria licha ya kuzaliwa nchini Ufaransa katika mji wa Sarcelles. Kwa sasa ndiye nahodha wa timu ya taifa ya Algeria pale Misri akiliwakilisha taifa lake vema.

Andre /Jordan Ayew (Ghana, wamezaliwa Ufaransa)

Watoto wa staa wa zamani wa kimataifa wa Ghana, Abeid Pele. Andre ambaye ni mkubwa pamoja na mdogo wake, Jordan wote walizaliwa nchini Ufaransa wakati huo baba yao akisakata soka katika nchi hiyo kwa mafanikio.

Wakati Andre alizaliwa katika mji wa Seclin, Jordan alizaliwa katika mji wa Marseille. Wote wameanza kuichezea Ghana tangu ngazi za vijana na kwa sasa Andre ndiye nahodha wa kikosi hicho ambacho kilitolewa na Tunisia katika hatua ya mtoano.

Ola Aina (Nigeria, kazaliwa England)

Mlinzi wa kushoto wa timu ya taifa ya Nigeria ambaye kwa sasa anacheza katika klabu ya Torino ya Italia. Aina alizaliwa katika jiji la London na wazazi wa Kinigeria na tayari aliichezea England katika ngazi zote za soka la vijana.

Hata hivyo, mwaka 2017 aliamua kutangaza kuichezea timu ya taifa ya Nigeria baada ya kushawishiwa kufanya hivyo na mabosi wa soka la Nigeria wakiongozwa na Rais wa soka nchini humo, Amaju Pinnick.

Achraf Hakim (Morocco, kazaliwa Hispania)

Mlinzi wa kushoto wa kimataifa wa Morocco ambaye anakipiga katika klabu ya Borussia Dortmund. Hakim alizaliwa katika jiji la Madrid nchini Hispania na wazazi kutoka Morocco, lakini tangu akiwa kijana aliamua kukipiga katika timu za taifa za vijana za Morocco. Kwa sasa ni panga pangua katika kikosi cha kwanza cha Morocco ambacho tayari kimeondoshwa katika michuano hii.

Yannick Bolasie (DRC, kazaliwa Ufaransa)

Staa mwingine wa Afrika ambaye alizaliwa Ulaya na alikuwa na uwezo wa kuchagua kucheza taifa moja kati ya matatu ya Ufaransa, England na Nigeria. Bolasie alizaliwa Ufaransa katika jiji la Lyon na wazazi kutoka Jamhuri ya Congo lakini alikulia zaidi England na mwisho akaamua kukipiga katika timu ya taifa ya Congo.

Eric Maxim Choupo-Moting (Cameroon, kazaliwa Ujerumani)

Staa huyu anayekipiga katika timu ya PSG ya Ufaransa alizaliwa jijini Hamburg nchini Ujerumani na baba Mcameroon wakati mama yake alikuwa Mjerumani. Aliwahi kukipiga katika timu za taifa za vijana za Ujerumani ngazi mbalimbali, lakini mwaka 2010 alitangaza kuichezea timu ya wakubwa ya Cameroon ambapo aliitwa katika kikosi kilichoshiriki Kombe la Dunia nchini Ujerumani. Kwa sasa ndiye nahodha wa kikosi cha Cameroon.

Medhi Benatia (Morocco, kazaliwa Ufaransa)

Mlinzi nguli wa Morocco. Alizaliwa katika eneo la Courcouronnes nchini Ufaransa na wazazi wa Kimorocco na mwaka 2005 alikuwa katika kikosi cha Ufaransa chini ya umri wa miaka 17. Hata hivyo, baadaye aliamua kujiunga na kikosi cha Morocco chini ya umri wa miaka 20 na kuanzia hapo alitinga katika kikosi cha wakubwa ambacho amekichezea kwa muda mrefu na sasa ni nahodha wao.

Moussa Marega (Mali, kazaliwa Ufaransa)

Nyota ambaye ameongoza mashambulizi katika kikosi cha Mali michuano ya mataifa ya Afrika mwaka huu. Marega alizaliwa Ufaransa katika kitongoji cha Les Ulis, lakini kuanzia mwaka 2015 aliamua kuichezea timu ya taifa ya Mali ambako wazazi wake walitoka na kuhamia Ufaransa.

Keita Balde (Senegal, kazaliwa Hispania)

Mtoto wa Senegal aliyezaliwa eneo la Arbucies nchini Hispania. Akiwa kijana, Balde ambaye amekuzwa na Barcelona, alichezea timu ya vijana ya jimbo la Catalunya lakini hatimaye Wasenegal walimshawishi na kukipiga katika timu yao ya taifa tangu mwaka 2017.

Advertisement