Mastaa 10 waliotikisa Simba, Yanga hawa hapa

Monday May 20 2019

 

By Charles Abel

Dar es Salaam. Ligi Kuu Tanzania Bara inaelekea ukingoni ambapo hadi sasa imefikia raundi ya 36 ingawa zipo timu zimecheza mechi chache zaidi ya hizo kutokana na kuwa na viporo ambavyo vilitokana na ratiba zao kubadilishwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).

Kumalizika kwa Ligi Kuu msimu huu ni mwanzo wa maandalizi kwa ajili ya msimu ujao kwani kunatoa fursa kwa timu kuanza kufanya usajili na kuingia kwenye kambi za mazoezi ili kuwa na vikosi imara vyenye ushindani msimu ujao.

Kwa wachezaji, ligi inapomalizika inaweza ikawa neema kwao kwa kuwa wanaweza kuvuna kiasi kikubwa cha fedha za usajili watakapojiunga na klabu nyingine au kuongeza mikataba kwenye timu wanazocheza.

Lakini kuna wale ambao huenda kikawa kipindi kigumu kwao kukosa timu za kuwasajili ama kutemwa na klabu zao kutokana na kiwango duni ambacho wameonyesha msimu huu, lakini hayo yote yatategemeana na ripoti zitakazowasilishwa na makocha wa timu zao.

Simba na Yanga ndio timu ambazo mara kwa mara zimekuwa zikishika na kutikisa dirisha la usajili kwani ndizo zimekuwa na misuli imara ya kiuchumi.

Orodha ya nyota 20 wa Simba na Yanga ambao kati yao 10 ni wale waliofanya vizuri zaidi kwenye Ligi Kuu msimu huu ambao wanaweza kuvuna fedha kutokana na kiwango chao bora walichoonyesha na wengine 10 ambao wamekalia kuti kavu kutokana na kutofanya vizuri.

Advertisement

WALIOFANYA VIZURI

John Bocco-Simba

Mkataba wa nahodha wa Simba, John Bocco unamalizika mwishoni mwa msimu huu baada ya kuitumikia timu hiyo kwa miaka miwili akitokea Azam FC kama mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake.

Amefunga mabao 14 kwenye Ligi Kuu msimu huu na kuonyesha kiwango bora hivyo na ni jambo lililo wazi kuwa klabu yake inajipanga kumuongeza mkataba mpya ambao bila shaka utakuwa mnono kwake kwani inasadikika kuwa Azam na Yanga zinamuwinda.

Emmanuel Okwi-Simba

Mkataba wake unaelekea ukingoni lakini ni wazi kwamba uongozi wa klabu hiyo na hata mashabiki wa Simba hawako tayari kumuona akiondoka kutokana na mchango ambao amekuwa akitoa kwa kikosi hicho.

Amefunga mabao 14 kwenye Ligi Kuu na inadaiwa kuna ofa mezani kutoka Afrika Kusini lakini viongozi wa Simba wanapambana kuhakikisha anabaki.

Meddie Kagere-Simba

Nani kama Kagere pale Simba? Msimu wake wa kwanza tu tayari ameshapachika mabao 20 yanayomfanya aongoze mbio za kuwania zawadi ya ufungaji bora wa ligi msimu huu.

Ligi ikimalizika atakuwa amebakiza mkataba wa mwaka mmoja lakini kuna uwezekano mkubwa Simba wakamuongezea mkataba mapema ili kumbakiza Mtaa wa Msimbazi.

Haruna Niyonzima-Simba

Alianza vibaya msimu kwa kuondolewa kwenye mipango ya kocha Patrick Aussems kufuatia kitendo chake cha kutokwenda na timu katika kambi ya maandalizi nchini Uturuki.

Hata hivyo, Niyonzima amegeuka lulu kikosini kutokana na kiwango bora ambacho amekuwa akionyesha kiasi cha kupewa nafasi katika kikosi cha kwanza na tayari Aussems ameshasisitiza kuwa kiungo huyo mshambuliaji aongezewe mkataba.

James Kotei-Simba

Mkataba wake unamalizika lakini dalili zipo wazi kuwa ataendelea kubaki ndani ya kikosi cha Simba kutokana na kazi kubwa anayofanya kwenye nafasi yake ya kiungo wa ulinzi.

Heritier Makambo-Yanga

Ni aina ya mchezaji ambaye mwanzoni wakati anakuja alionekana kama mchezaji wa daraja la kawaida kwa namna usajili wake ulivyofanyika lakini baada ya kuanza kuitumikia timu hiyo, amegeuka mkombozi wa Yanga msimu huu.

Ameiweka Yanga mgongoni kwa kupachika mabao 16 ambayo mengi kati ya hayo, yaliamua matokeo ya timu hiyo kwa kupata pointi tatu muhimu kwenye mchezo husika.

Paul Godfrey ‘Boxer’

Ni kinda aliyepandishwa kutoka kwenye kikosi cha vijana cha Yanga na amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kucheza vyema nafasi ya beki wa kulia na kuwafanya mashabiki wamsahau beki Juma Abdul.

Dalili ziko wazi kwamba Yanga hawatakuwa tayari kuona akiondoka, hivyo anajiandaa kuvuta donge nono mwishoni mwa msimu.

Ibrahim Ajibu-Yanga

Mkali wa kupiga pasi za mwisho kwenye Ligi Kuu akiwa amefanya hivyo mara 16 huku pia akiwa amefunga mabao sita na mchango wake uliifanya hadi Yanga kumpa kitambaa cha unahodha.

Mkataba wake na Yanga unamalizika mwishoni mwa msimu na wameonyesha nia ya kumbakiza ingawa  Simba nao wanamuwinda ili wamrudishe Msimbazi.

Papy Tshishimbi-Yanga

Anaelekea kumaliza mkataba lakini amekuwa muhimili wa Yanga kwenye safu ya kiungo kutokana na jinsi anavyounganisha na kuchezesha timu,   pia amekuwa akifunga mabao katika baadhi ya michezo.

Tshishimbi ametajwa kuwaniwa na Simba, lakini hakuna uwezekano wa Yanga kumuachia kwa urahisi.

Abdallah Shaibu ‘Ninja’

Amekuwa tegemeo katika safu ya ulinzi ya Yanga jambo lililomfanya apate namba ya kudumu kutokana na jitihada zake za kuwadhibiti washambuliaji wa timu pinzani.

Waliochemsha

Buruhani Akilimali-Yanga

Alisajiliwa na kocha George Lwandamina kwa mbwembwe lakini msimu huu amejikuta akisotea benchi huku akicheza mechi moja tu.

Adam Salamba-Simba

Licha ya kufunga mabao manne, anaonekana kutoaminika na benchi la ufundi la Simba ambalo limekuwa halimpi nafasi ya kutosha ya kucheza na kuna taarifa kuwa atatolewa kwa mkopo ili kupisha usajili wa mshambuliaji mpya mzawa.

Zana Coulibaly-Simba

Alisajiliwa kwa lengo la kuziba pengo la Shomary Kapombe ambaye aliumia lakini ameonyesha kiwango cha kawaida tofauti na matarajio ya wengi na kimekuwa hakitabiriki.

Juma Abdul-Yanga

Nafasi yake inachezwa vyema na kinda Paul Godfrey na amekuwa muda mrefu akisugua benchi huku kukionekana hakuna dalili kwake kurudi moja kwa moja kwenye nafasi yake.

Pius Buswita-Yanga

Majeraha yameonekana kumrudisha nyuma kwani muda mwingi amekuwa akijiuguza lakini pia anaonekana kutofiti kwenye mfumo na mbinu za kocha Mwiny Zahera ambaye amekuwa hampi nafasi ya kutosha kucheza.

Nicholas Gyan-Simba

Alisajiliwa kama mshambuliaji wa pembeni lakini baadaye alibadilishwa nafasi na kuchezeshwa kama beki wa kulia.

Nafasi hiyo inaonekana inampa taabu Gyan ambaye amekuwa hana nafasi ya kudumu kikosini na yupo kwenye orodha ya nyota watakaotemwa ili kupisha usajili mpya.

Asante Kwasi-Simba

Alianza vyema ndani ya kikosi cha Simba lakini baadaye akaja kupoteza namba mbele ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na kila anapopewa nafasi amekuwa akichemsha.

Mateo Anthony-Yanga

Amefunga bao moja tu kwenye Ligi Kuu msimu huu na amekuwa hapati nafasi kikosini akijikuta akitazama mechi akiwa jukwaani ama akisotea benchi.

Haji Mwinyi-Yanga

Kwa  misimu miwili mfululizo, amekuwa akisotea benchi ndani ya kikosi cha Yanga, akishindwa kumpoka namba Gadiel Michael ambaye amekuwa akiaminiwa na benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Zahera.

Ally Salim-Simba

Kipa Ally Salim ambaye amepandishwa kutoka katika kikosi cha vijana cha Simba, amekuwa hapewi nafasi kwenye timu ya wakubwa kutokana na uwepo wa makipa Aishi Manula na Deogratias Munishi ‘Dida’.

Inadaiwa kuwa Simba inamuwinda kipa Beno Kakolanya ambaye ni mchezaji huru kwa sasa na ikiwa atatua, basi Salim anaweza kutolewa kwa mkopo ili apate timu itakayompa nafasi ya kucheza.

Advertisement