VIDEO: Masharti mazito ligi nne zikirejea

Friday May 22 2020

By Edwin Mjwahuzi

Wakati ikitangaza kurejea kwa mashindano manne ya soka, Serikali imeweka masharti kadhaa yanayotakiwa kufuatwa na wadau na mamlaka nyingine zinazosimamia mchezo huo nchini.


Mashindano hayo ni Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Azam Sports Federation, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la pili.


Akizungumza katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dodoma leo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe alisema kuwa ligi hizo nne zinazorejea ni hatua ya awali ya kurudisha shughuli nyingine za michezo kama ilivyoagizwa na Rais Dk. John Magufuli jana.
"Baada ya mkuu wa nchi kuelezea kwamba ana nia ya kuruhusu baadhi ya shughuli za jamii kuendelea kufanyika, sisi wizara haraka kabisa tukaanza vikao vya kujiandaa.
Je mkuu wa nchi akisema tunaanza wiki ijayo tunafanyaje?Tulikaa vikao na mimi nikawapa wataalamu wangu hadidu za rejea.Kwanza watambue kwamba klabu zetu za mpira ziko hoehae kiuchumi.


Ule utaratibu wa zamani timu inatoka Songea kwenda Mara na baada ya hapo kwenda kwingine hawatoweza lazima tulitambue kwa sababu hawana kipato, ligi ilisimama na wakawa wanalipa wachezaji," alisema Waziri Mwakyembe.


Waziri Mwakyembe alisema pindi mashindano hayo yatakaporejea, taratibu kadhaa ni lazima zifuatwe ili kuepuka uwezekano wa maambukizi ya virusi vya Corona vinavyosabisha ugonjwa wa Covid 19.
"Mapendekezo waliyoniletea makuu ni kwamba ebu tufungulie michezo kwa tahadhari kwa hiyo tunafungulia ligi nne kwa kuanzia na tukienda vizuri tutafungulia kote.


Kila timu tutaruhusu iwe na idadi kadhaa ya washangiliaji, kumi au ishirini ili wenzetu wanaocheza pale wajue kwamba kuna watu wanawaangalia.
Tuangalie pia kama viwanja vinavyotumika viwe na magari ya wagonjwa na wataalam wa huduma ya kwanza kwa ajili sio ya Covid 19 bali hata watu wakiumia watibiwe," alisisitiza Waziri Mwakyembe.

Advertisement


Waziri Mwakyembe alisema pia wachezaji hawatoruhusiwa kusalimiana kwa kushikana mikono, kutema mate mara kwa mara, kushangilia kwa kukumbatiana lakini pia mashabiki kutojazana ndani na nje ya viwanja.


Mashindano ya soka na michezo mingine, vilisimamishwa tangu Machi 17 mwaka huu ikiwa ni miongoni mwa hatua za serikali kukabiliana na virusi vya Corona.

Advertisement