Martinelli aanza kwa kishindo, Arsenal yaua

Tuesday July 16 2019

 

London, England. Mshambuliaji chipukizi wa Arsenal, Gabriel Martinelli ameanza kwa kishindo baada ya kufunga bao moja katika ushindi mabao 3-0 dhidi ya Colorado Rapids katika mchezo wa kirafiki wa kujianda na msimu mpya.

Mshambuliaji Martinelli mwenye miaka 18, amesajiliwa kwa gharama ya pauni 6milioni kutokea katika klabu ya Ituano FC ya Brazil, alifunga bao akiunganisha krosi ya Dominic Thompson katika dakika 61.

Mabao mengine ya Arsenal yalifungwa na Bukayo Saka na James Olayinka na kuwafanya Gunners kuanza msimu wa maandalizi Marekani kwa kishindo.

Martinelli alikuwa katika kiwango cha juu katika mchezo huo, alipoteza nafasi kadhaa za kufunga katika dakika tano za mwanzo za mchezo huo.

Chipukizi mwenye miaka 17, Saka alifunga bao la kwanza kwa Arsenal katika dakika 13, akitumia vizuri uzembe wa kipa wa Colorado, Clint Irwin kushindwa kudaka mpira uliopigwa na Eddie Nketiah, kabla ya Olayinka kuongeza la pili dakika 16.

Kocha Unai Emery aliwaanzisha wachezaji wengi chipukizi katika mchezo huo, huku Mesut Ozil, Pierre-Emerick Aubameyang na Alexandre Lacazette wakiingia katika dakika za mwisho.

Advertisement

Arsenal inaendelea na maandalizi yake pamoja na kujiandaa na michuano ya International Champions Cup ambako watacheza dhidi ya Bayern Munich, Fiorentina na Real Madrid jijini Los Angeles, huku mchezo dhidi ya Charlotte utachezwa Washington DC.

Advertisement