Man City yagomewa kuhusu medali mpya

Muktasari:

Utaratibu wa Ligi Kuu England ni kwamba medali ya ubingwa hutolewa kwa kila mchezaji aliyecheza kuanzia mechi tano za ligi hiyo, lakini kwenye kikosi cha Man City kwa msimu uliopita kuna wachezaji sita wa timu ya vijana walikosa medali licha ya kwamba walikuwa kwenye mazoezi ya kila siku ya kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

LONDON, ENGLAND. MAOMBI ya Manchester City kupata medali za ziada za ubingwa wa Ligi Kuu England yamepigwa chini ya wahusika, wakisema medali zinazotolewa zinajitosheleza.

Kikosi hicho cha Kocha Pep Guardiola baada ya kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu England msimu uliopita, ilitaka wachezaji wake wote wa kikosi cha kwanza wavae medali za ubingwa, lakini kuna waliokosa.

Man City ilipewa medali 40 za ubingwa kutolewa kwa wachezaji na wafanyakazi wengine waliohusika kwa msimu mzima kwenye mchakamchaka wa kusaka ubingwa.

Lakini, taarifa zinadai Man City ilitaka medali za ziada, ombi ambalo limekataliwa na Ligi Kuu England ikiamini medali zilizotolewa zinatosha.

Utaratibu wa Ligi Kuu England ni kwamba medali ya ubingwa hutolewa kwa kila mchezaji aliyecheza kuanzia mechi tano za ligi hiyo, lakini kwenye kikosi cha Man City kwa msimu uliopita kuna wachezaji sita wa timu ya vijana walikosa medali licha ya kwamba walikuwa kwenye mazoezi ya kila siku ya kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Kocha Guardiola amekerwa na kigezo hicho cha mchezaji kucheza mechi tano ndio apewe medali timu yake inaposhinda ubingwa, akisema: “Hiki kitu nakiona cha hovyo sana upande wangu. Kama wanataka medali yangu, nitawapa. Wao ni mabingwa, walifanya kazi na sisi kuanzia siku ya kwanza hadi ya mwisho, mazoezini na kwenye vyumba vya kubadilishia.

“Labda pengine ghali sana kwa Ligi Kuu England kutoa medali tatu, nne au tano kwa wachezaji makinda,” alisema.