Makocha Savio, ABC watunishiana msuli nusu fainali RBA

Muktasari:

Katika mechi ya mkondo wa kwanza Savio ilishinda pointi 53-50 na mechi ya mkondo wa pili ABC ilishinda pointi 66-51.

Dar es Salaam.Wakati mashabiki wa mpira wa kikapu wakihesabu saa kujua hatma ya bingwa mtetezi wa Ligi ya mpira wa kikapu mkoa wa Dar es Salaam (RBA), Savio, kocha wa timu hiyo, Wiliam Mziray na mwenzake wa ABC Haleluya Kavalambi wametunishiana msuli kuelekea kwenye mchezo huo.

Savio na ABC zitacheza mechi ya tatu ya kuamua timu itakayofuzu nusu fainali ya RBA, mchezo utakaopigwa saa 12 jioni ya leo Jumanne kwenye Uwanja wa Don Bosco, Dar es Salaam.

Awali timu hizo kila moja ilishinda mechi moja kwenye robo fainali kna kulazimika kukutana kwenye gemu ya tatu ya kuamua mshindi atakayecheza na Kurasini Heat kwenye nusu fainali, huku Vijana ikicheza na Ukonga Kings.

"Ni mechi ngumu ambayo sisi tunaichukulia kama ya kufa na kupona, ingawa Savio ya sasa si kama ile ya miaka ya nyuma hivyo lazima tuwafunge," lijinasibu Kavalambi kocha wa ABC.

Alisema gemu ya kwanza walipoteza kwa tofauti ya pointi tatu, lakini walijipanga na gemu ya pili wakachomoza na ushindi wa zaidi ya pointi 15, hivyo wanaamini gemu ya tatu itakuwa yao.

"Tuko vizuri, timu ina morali japo mchezaji wetu, Mosses Jackson ni majeruhi lakini tuna mbadara wake," alisema.

Kocha Mziray wa Savio amesema wamejipanga kushinda mechi hiyo na kufuzu kucheza nusu fainali na fainali.

"Tunahitaji kutetea ubingwa wetu, hicho ndicho kitu ambacho kila mtu kwenye kikosi hiki anakiwaza, tunaamini tutashinda mchezo huu kwani hatuna historia ya kufungwa na ABC zaidi ya mechi iliyopita ambayo tulifanya makosa kidogo yaliyotugharimu," alisema.