Makamba ajitosa kuchangia Yanga

Muktasari:

  • Yanga inaongoza msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 74 katika michezo 32 iliyocheza huku kocha mkuu, Mwinyi Zahera akisisitiza kutaka ubingwa msimu huu licha ya kupewa presha na Simba yenye pointi 66 katika michezo 25 iliyocheza.

Dar es Salaam. Licha ya kuwa shabiki kindakindaki wa Simba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, January Makamba amesema timu hiyo haipaswi kuwabeza wapinzani wao Yanga katika kipindi wanachopitia sasa.

Yanga inakabiliwa na mtikisiko wa uchumi uliopelekea klabu hiyo kutumia utaratibu wa kuwashirikisha wanachama na mashabiki wao kuwachangia.

"Sio vibaya klabu kutafuta msaada kwa wanachama na ndicho inakifanya Yanga, ingawa Simba hatupaswi kuwabeza kwa kipindi wanachopitia," amesema Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli.

Amesema yeye licha ya kuwa shabiki na mwanachama wa Simba, lakini haoni tabu kuwachangia watani zao Yanga.

"Nitachanga si chini ya Sh 1 milioni, hakuna Simba imara bila Yanga imara," amesema Makamba Leo Aprili 24 alipotembelea makao makuu ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Tabata Relini jijini Dar es Salaam.

Amesema Yanga licha ya changamoto wanazopitia, lakini inafanya vizuri na matokeo yanaonekana kwani timu inapambana.