Magori : Hiki ndio kinachoua soka la bongo

Muktasari:

Tukienda viwanjani hatuangalii timu inachezaje wakati inapopoteza, mpira tunaangalia mara nyingi wakati timu ina mpira, kuna wachezaji timu haina mpira wanatembea tu na hao ndio wale tunaowapenda sana.

KATIKA mfululizo wa makala za Crescentius Magori, aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Simba na Mshauri Mkuu wa sasa wa Bilionea wa klabu hiyo, Mohammed Dewji, jana Jumatatu alifunguka jinsi walivyoteswa na tuhuma kwamba Simba hupulizia dawa za kuwanyong’onyeza wapinzani katika vyumba vya kuvalia ama hoteli wanazofikia. Endelea.

SOKA LETU LINAKWAMA WAPI?

“Hatuwekezi tunatumia tu, ndio tatizo kubwa la mpira wetu, hatuweki mpira katika maendeleo. Angalia bajeti ya Yanga pia nenda ya Simba angalia katika zile timu za watoto kuna kiasi gani kimetengwa kwa eneo hilo? Ukitoka hapo angalia timu za wakubwa pia angalia hao wachezaji wanapatikana wapi? Tulimuona yule Mwamnyeto (Bakari). Wako wengi tu, lakini wanavunwaje wale wakiwa huko walipo?

“Soka letu linapenda sana wale wachezaji wanaopiga chenga, kanzu na matobo ambao mara nyingi hawana faida kubwa kwenye timu. Tukienda viwanjani hatuangalii timu inachezaje wakati inapopoteza, mpira tunaangalia mara nyingi wakati timu ina mpira, kuna wachezaji timu haina mpira wanatembea tu na hao ndio wale tunaowapenda sana.

“Ile Simba ambayo tuliwatoa Zamalek tulikuwa na wachezaji bora washindani, Pawasa (Boniface), Matola (Seleman), Kaseja (Juma) walikuwa hawataki kusikia timu inafungwa. Kila ukiongea nao wanakwambia tunashinda. Hao ndio wachezaji washindani. Wachezaji wetu wa sasa, hakuna kitu nachukia kama ukisikia wanahojiwa, utasikia ‘mpira una matokeo matatu kufungwa, kushinda na sare’.

“Ukimsikia hivyo ujue huyo sio mshindi. Mtafuteni yule Mbrazil Fraga (Gerson) kama kuna kitu hataki kusikia basi ni kufungwa hao ndio wachezaji wa ushindi.”

MASHABIKI WANAKOSEA SANA

Kuhusu lawama kwa nyota wanaosajiliwa, Magori anasema; “Kuna kosa moja sisi Watanzania tunafanya kila wakati kuwahi kuwahukumu wachezaji hatujifunzi kabisa. Hii tabia yetu ya kuwahi kuwahukumu mapema wachezaji ni kitu kibaya sana. Kosa hili tunalifanya karibu kila mwaka. Mfano mzuri ni Okwi (Emmanuel) wakati anafika bahati nzuri presha ya usajili haikuwa kubwa kiasi hiki.

“Okwi wakati anafika ule mwaka wa kwanza ilikuwa hovyo kabisa, sikumbuki hata kama alifunga mabao mawili kwenye ligi, kuna mechi moja nakumbuka Simba ilianzia ligi ugenini tulianzia Majimaji, kule Songea kisha tukaja Mbeya, tena siku hiyo Okwi alianza ingawa hakumaliza. Kuna jamaa mmoja anaitwa Kipukuswa ni shabiki wa soka, akanipigia simu anauliza huyu Okwi mtoto mdogo mmemtoa wapi huyu? Anarukaruka tu humu. Sikumbuki hata kama alimaliza mechi. Nakumbuka Simba tulishinda bao 1-0 lilifungwa na Naftali (David). Hiyo mechi tulizidiwa sana lakini lawama kubwa zilikuwa ni Okwi.

“Tukarudi Dar es Salaam akashindwa kucheza karibu msimu mzima. Msimu uliofuata sasa akaanza kubadilika kila mtu alianza kushangaa. Hivyo utaona sisi Watanzania tulivyo na hulka ya kuwahi kuhukumu mapema wachezaji na hata makocha. Unawezaje kumjadili mchezaji na kusema huyu hafai ndani ya mechi chache?”

“Nafahamu kuna wachezaji wanafanikiwa kukubalika kwa haraka. Unajua kuna mchezaji anaweza kuja kwenye timu yako baada ya nusu saa anakuwa kama ameishi hapo mwaka mzima, kuna wengine watachukua wiki mwezi na hata miezi,” anasema na kuongeza;

“Binadamu tuko tofauti sana, kuna wengine sisi mazingira kuzoea inachukua muda na wengine ndani ya muda mfupi anakuwa yuko sawa. Hebu kumbukeni alivyokuja Tshishimbi (Papy Kabamba)tena amekuja siku kama tatu kabla ya mechi ya Simba na Yanga, akacheza vizuri kuliko yeyote uwanjani siku hiyo, mnakumbuka ile mechi?

“Klabu yake ilipambana huko kukamilisha usajili wake akaja Yanga walikuwa Pemba huko, akaingia uwanjani. Angekuwa mwingine hata kugusa mpira angeshindwa. Wachezaji wanatofautiana.

USAJILI WA KILA MSIMU

Alipoulizwa inakuwaje klabu za Simba na Yanga zinafanya usajili kila msimu na haoni kama una athari zake, naye anajibu;

“Uhitaji wa timu, unajua kama nilivyosema huko nyuma, Simba kwa mfano mwaka huu katika mabadiliko ya timu yetu katika usajili tulikuwa tunaangalia wachezaji ambao watakuja kutupa makubwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika na matatizo yetu tulishaambiwa ni yapi, ukiangalia hata mabao ambayo tulifungwa katika mechi za ugenini Afrika yote yalikuwa na ufundi mkubwa.

“Zinapigwa kona wachezaji wetu wanasimama hawaruki, zinapigwa adhabu ndogo watu hawakabi mpira, huna wachezaji wagumu kupambana kwahiyo sasa huwezi kusema usifanye usajili, kwani watu watasema tulilazimika kutafuta watu bora zaidi ya wale tuliokuwa nao, mnaweza msione sasa tutakapokuja kukutana na timu ngumu zenye wachezaji bora ndio mtakuja kutambua aina ya usajili wetu.

FRIENDS OF SIMBA BADO WAPO?

“Ipo lakini nguvu yake imepungua kwasababu, sasa hivi timu kiuchumi ipo vizuri, unajua Friends of Simba ilikuwa na nguvu sana wakati ule kutokana na wao ndio waliokuwa wanachanga kila kitu, tulikuwa na taarifa za makusanyo ya michango ya kila mwezi kwa kila mwanachama wa kundi hili na hapo tulikuwa hatuangalii una pesa kiasi gani. Ilikuwa kila mmoja ana kiwango chake anachoweza kutoa kwa mwezi mwenye uwezo wa milioni moja au zaidi, chini yake hakuna tatizo. Tulikuwa tuna watu wanatoa hadi Sh 20,000.

“Ukiwa mwezi flani hujatoa unakumbushwa bwana kuna madeni yako huku, ukiweza unatoa maisha yanaendelea. Sasa hizi fedha ndizo zilikuwa zinakuja kusaidia timu. Mfano ikifika mechi kubwa tunajikusanya na kupitisha michango tena. Tukimaliza tunawafuata wachezaji tunawapa ahadi yetu, mkishinda tutawapa mfano Sh.30 milioni na klabu nayo inasema itatoa Sh.50 milioni jumla Sh.80 milioni na hapo ndipo tulipokuwa tunawaumiza Yanga hata wakati ambao alikuwepo Manji (Yusuf).

WACHEZAJI WANADAI ADA ZA USAJILI?

“Nimefurahi ulivyoniuliza hili swali, timu hii ya sasa ilisajiliwa mimi nikiwa mtendaji, nasema leo, hakuna mchezaji Simba anayedai ada ya usajili hata mmoja, unajua Simba kwanza utaratibu wetu tuliubadilisha sana katika kusajili, kwanza hatulipi fedha taslimu kabisa isipokuwa msimu huu tulifanya kwa mchezaji mmoja pekee Deo Kanda.

“Tulipomaliza kumsajili tukamwambia afungue akaunti tumuingizie fedha zake, aligoma. Tukamalizana.”