Madrid wanena ‘bado Pogba sasa’

Muktasari:

Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane anamtaka staa huyo ambaye ni Mfaransa mwenzake na Machi mwaka huu aliweka wazi kwamba anavutiwa na kiwango cha Pogba huku Pogba mwenyewe akikiri ndoto yake ni kucheza Real Madrid siku moja.

MADRID,HISPANIA.REAL Madrid imeamua dirisha hili. Inaonekana imeamua kuingia sokoni kwa ajili ya kukisuka upya kikosi chake baada ya kuumbuka msimu huu. Na sasa inadaiwa imeanzisha mazungumzo rasmi na Manchester United kwa ajili ya kumnasa Paul Pogba.

Mabosi wa Madrid walikutana na wenzao wa Mashetani Wekundu wiki iliyopita kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kumchukua Pogba wakati wakiwa London kukamilisha uhamisho wa staa wa Chelsea, Eden Hazard ambaye wamekwishamtangaza.

Hata hivyo, United inataka faida huku ikitaka kumuuza kiungo huyo wa kimataifa wa Ufaransa kwa dau la Pauni 150 milioni baada ya kumnasa kwa dau la Pauni 89 milioni katika dirisha kubwa la majira ya joto mwaka 2016.

Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane anamtaka staa huyo ambaye ni Mfaransa mwenzake na Machi mwaka huu aliweka wazi kwamba anavutiwa na kiwango cha Pogba huku Pogba mwenyewe akikiri ndoto yake ni kucheza Real Madrid siku moja.

Uwezekano wa Pogba kukipiga Madrid umezidi kuonekana kutokana na kudorora kwa uhusiano na kocha wake wa sasa, Ole Gunnar Solskjaer baada ya awali kutokuwa na uhusiano mzuri na kocha aliyepita, Jose Mourinho.

Pogba pia alikwaruzana na mashabiki wa United katika pambano la mwisho la msimu dhidi ya Cardiff City Old Trafford baada ya United kuchapwa mabao 2-0 na mashabiki walimwambia Kocha Solskjaer amuuze kama kuna uwezekano huo.

Mapema wiki iliyopita, mmoja kati ya waandishi wakongwe wa soka la Hispania, Eduardo Inda alikiambia kituo kimoja cha televisheni nchini humo kuwa Madrid inatazamiwa kumfuata Pogba baada ya kumalizana na Hazard huku akitoboa siri kuwa Pogba amekubali kukatwa mshahara wake ili kukamilisha dili hilo.

“Dili la Pogba ni kama vile limekamilika. Wa kwanza kununuliwa atakuwa Hazard kisha Pogba. Amekubali kukatwa mshahara kutoka aliokuwa analipwa na Manchester United Pauni 13 milioni kwa mwaka hadi Pauni 10 milioni,” alisema Inda.

“Adidas wanalazimisha sana aende kwa sababu ni mmoja kati ya wachezaji wao wakubwa ambao wanawatangazia bidhaa zao. Nadhani dau lake la kumnunua linaweza kuwa Pauni 137 milioni hadi 150 milioni,” aliongeza Inda.

Real Madrid inataka kumtumia winga wake wa kimataifa wa Wales, Gareth Bale kama chambo kwa ajili ya kumnasa Pogba na inaamini United itakubali kupokea pesa pamoja na kumchukua Bale ambaye hatakiwi na Zidane kwa sasa.

Kuwasili kwa Hazard Santiago Bernabeu kumefuta kabisa nafasi ya Bale katika kikosi cha Real Madrid baada ya Zidane kukiri katika mechi za mwisho za Madrid msimu uliopita anataka kuitengeneza Madrid mpya.

Tayari Madrid pia imefanikiwa kumnasa mshambuliaji mahiri wa kimataifa wa Serbia, Luka Jovic kutoka Frankfurt ya Ujerumani kwa dau la Pauni 62 milioni ambalo linamfanya kuwa mshambuliaji ghali katika historia ya klabu hiyo.

Madrid pia inakaribia kumchukua beki wa kushoto wa Lyon na Timu ya Taifa ya Ufaransa, Ferland Mendy kwa dau la Pauni 44 milioni na tayari klabu hizo mbili zimeshakubaliana dau la uhamisho la staa huyo huku uhamisho wake ukitarajiwa kutangaza leo Jumatatu.

Madrid pia imekuwa ikihusishwa na kiungo mchezeshaji wa Tottenham, Christian Eriksen ambaye anaweza kupatikana kwa bei nafuu wakati huu akiwa amebakiza miezi 12 katika mkataba wake na Spurs.

Msimu uliopita Real Madrid haikuambulia taji lolote na badala yake ilipoteza taji lake la Ulaya baada ya kuchapwa kwa aibu na Ajax.