Mabao 10 bora ya Hazard Chelsea

Wednesday June 12 2019

 

LONDON,ENGLAND. HATIMAYE kisiki, Eden Hazard kimeng’oka Chelsea na kwenda Real Madrid kwa uhamisho wa Pauni 115 milioni. Hazard amefanya mambo mengi makubwa na amefunga mabao mengi ya kukumbukwa.

Yafuatayo yanaweza kuwa mabao 10 bora ambao Hazard aliwahi kuifungia klabu yake hiyo.

Hazard vs Everton (EPL, Novemba, 5, 2016)

Hili lilikuwa bao la kitimu ambalo lilimaliziwa kwa kazi nzuri binafsi ya Hazard. Katika pambano hili dhidi ya Everton, wachezaji wa Chelsea walipiga pasi 23 kabla ya mpira kumwangukia Hazard ambaye alimkwepa vyema beki wa Argentina, Ramiro Funes Mori kabla ya kuingia katikati na kumtingisha beki Ashley Williams kisha kupiga shuti la chinichini lililompita kipa, Maarten Stekelenburg.

Lilikuwa bao la nne la Chelsea ndani ya dakika 56 tu huku pambano likimalizika kwa ushindi wa mabao matano wa Chelsea.

Hazard vs Stoke City (EPL, Januari 12, 2013)

Advertisement

Mara zote tumemzoea Hazard ambaye anafunga mabao mengi baada ya kupiga chenga ambazo anaingia nazo mpaka katika boksi la adui.

Katika pambano hili dhidi ya Stoke City, Hazard aliamua kuchukua maamuzi mengine binafsi. Alisogea na mpira akivuka katika ya uwanja kwenda katika lango la Stoke.

Kwa umbali wa mita 30 alipiga shuti kali lililompita kipa, Asmir Begovic kama umeme. Lilikuwa bao la nne katika ushindi wa 4-0 wa Chelsea ugenini.

Hazard vs Liverpool (Ligi, Desemba 29, 2013)

Bao jingine ambalo lilidhihrisha umakini wa staa huyu wa kimataifa wa Ubelgiji katika umaliziaji. Pasi nzuri ya kiungo wa Brazil, Oscar ilizuiwa na beki wa Kifaransa, Mamadou Sakho lakini mpira ukamuangukia Hazard.

Bila ya kusita na wala kutuliza alipiga shuti la mkato na mpira ukaenda juu kushoto mwa lango la kipa, Simon Mignolet ambaye ni Mbelgiji mwenzake. Bao maridadi. Staa wa Cameroon, Samuel Eto’o akafunga bao la pili la ushindi katika kikosi hicho la Kocha Jose Mourinho.

Hazard vs Liverpool (Ligi, Mei 11, 2016)

Msimu wa 2015/16 ulikuwa ni mbaya na wa kusahauliwa kwa Hazard. Alifunga mabao manne tu ya msimu huku bao lake la kwanza akifunga Aprili mwaka huo.

Hata hivyo, bao lenyewe lilikuwa la kusisimua sana. Alitokea upande wa kushoto kama kawaida yake, akamvuka Adam Lallana, akawapita Roberto Firmino na James Milner, kabla ya kupiga shuti la mkato mbele ya Dejan Lovren na mpira ukaenda moja kwa moja nyuma ya nyavu za kipa Simon Mignolet. Bonge la bao.

Hazard vs Manchester United (FA, Machi 10, 2013)

Katika pambano hili la robo fainali za FA, Chelsea ilikuwa imelala mabao 2-0 Old Trafford wakati Hazard alipoingizwa uwanjani kwa ajili ya kuikoa timu yake. Kweli alifanya hivyo.

Ikiwa imebakia saa moja pambano kumalizika, Hazard kama kawaida yake aliupata mpira kushoto mwa uwanja akiwa na akili moja tu kufunga mwenyewe.

Akakabiliana na beki wa kulia wa Manchester United, Mbrazili Rafaael lakini akauzungusha katika mbavu za Rafael na mpira huo kwenda moja kwa moja katika nyavu za United akimwacha kipa David de Gea asiwe na cha kufanya.

Hazard vs Watford (Ligi, Februari 5, 2018)

Baada ya kuchukua ubingwa msimu mmoja kabla ya hapo, Chelsea ilijikuta katika msimu mgumu wa 2017/18 lakini hata hivyo, haikumzuia Hazard kuendelea kufanya maajabu yake. Katika pambano hili dhidi ya Watford, Chelsea ilikuwa imechapwa bao moja wakati Hazard alipoamua kutumia maajabu yake binafsi kusawazisha katika dakika ya 82.

Kwanza alianza kwa kumhepuka beki Adrian Mariappa kisha kumzunguka tena kabla ya kupiga shuti kali la chini lililomwacha kipa, Orestis Karnezis akiwa hana la kufanya.

Hazard vs Sparta Prague (Europa Februari 21, 2013)

Dalili za awali za kipaji kikubwa cha Hazard alipotua katika Ligi Kuu ya England ilikuja mwanzoni tu wakati alipocheza pambano la kwanza la msimu dhidi ya Sparta Prague michuano ya Europa baada ya kutolewa katika makundi Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Huku pambano hilo likionekana kuelekea katika dakika za nyongeza, Hazard kama kawaida yake alipokea mpira katika winga moja kuelekea katika lango la Sparta. Baada ya kuwaacha mabeki wawili wa Sparta alipiga shuti kali karibu na mwamba wa lango huku mpira ukitinga nyavuni.

Bao hilo liliipeleka Chelsea katika hatua ya 16 bora. Bahati mbaya kwake katika siku za usoni, Hazard alilikosa pambano la fainali kutokana na majeraha lakini alikuwa amechangia kuipeleka Chelsea fainali hizo.

Hazard vs Tottenham (Mei, 2, 2016)

Bao jingine la kukumbukwa kutoka kwa Hazard. Kwanza ni kwa uzuri wake lakini pia lilikuwa linaweka historia nzuri kwa Leicester City katika msimu maarufu wa 2015/16. Lilikuwa bao tamu baada ya Hazard kumpita Erik Lamela, kisha Kyle Walker halafu Eric Dier na baadae akapiga pasi kwa Diego Costa ambaye alimrudishia tena Hazard aliyepiga shuti kali la mkato lililompita kipa, Hugo Lloris.

Bao hilo lilikuwa linaufanya ubao wa matokeo kusomeka 2-2 na hivyo kuiondoa Tottenham katika mbio za ubingwa huku Leicester City ikikaribia kuchukua ubingwa. Ni pambano ambalo lilimalizika kwa vurugu kubwa kutokana na ubabe mwingi baina ya wachezaji uwanjani.

Hazard vs Arsenal (Ligi, Februari 4, 2017)

Moja kati ya mabao bora ambayo Hazard amewahi kuyafunga katika soka. Hili hapa. Katika pambano hili dhidi ya Arsenal, Hazard alikuwa anaihakikishia Chelsea kushika nafasi ya pili. Alipata mpira katikati ya uwanja akamzidi nguvu beki, Laurent Koscielny kisha kukwatuliwa kidogo na kiungo, Francis Coquelin lakini bado akayumba na kusimama imara.

Kwa mara ya pili Koscielny alijitokeza mbele yake lakini akampita kisha kupiga shuti lake lililompita kipa, Petr Cech. Moja kati ya mabao bora ya juhudi binafsi katika historia ya Ligi Kuu ya England. Chelsea ilishinda mabao 3-1 na mwisho wa msimu ilichukua ubingwa.

Hazard vs Liverpool (EFL, Septemba 26, 2018)

Bao jingine ambalo Hazard alifunga kwa juhudi binafsi. Hili ni moja kati ya bora kabisa. Wakati mechi ikiwa inaeelekea katika dakika za nyongeza, Hazard alipata mpira nje kabisa ya lango la Liverpool kabla hajaanza kuwageuza mastaa wa Liverpool, mmoja baada ya mwingine.

Alianza kuwatoroka viungo, Jordan Henderson na Fabinho kisha akacheza ‘one two’ na Cesar Azpilicueta kabla ya kumpiga tobo Roberto Firmino. Akasogea tena mbele kwa staili ileile na kukutana na kiungo wa Guinea Naby Keita kisha kumgeukia Alberto Moreno kabla ya kupiga shuti kali lililompita kipa, Simon Mignolet. Bao jingine dhidi ya kipa huyu raia mwenzake wa Ubelgiji ambaye amekuwa mhanga wa ubora wa Hazard mara nyingi. Bao safi.

Advertisement