MO Dewji, mastaa Simba wambeba Sven

BAADHI ya mashabiki wa Simba hawajafurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na timu hiyo katika mechi mbili za kirafiki na lawama kubwa wakizielekeza kwa benchi la ufundi chini ya Kocha Sven Vandenbroeck.

Kutumia mfumo wa kuchezesha mshambuliaji mmoja tu wa kati lakini pia kutompa nafasi ya kutosha ya kucheza mshambuliaji wao nyota Medie Kagere katika mechi mbili za mwanzo za Ligi Kuu dhidi ya Ihefu na Mtibwa Sugar yanaelezwa kama sababu za mashabiki hao kutokuwa na imani na kocha huyo.

Hata hivyo, wakati mashabiki hao baadhi wakionyesha kutokuwa na imani na benchi lao la ufundi, mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Simba, Mohammed Dewji na mastaa wa zamani wa klabu hiyo wamewataka mashabiki hao kuwa na utulivu na kuweka imani kwa Vandenbroeck na benchi lake la ufundi wakiamini timu hiyo itakaa sawa.

Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii na zile za Simba, Dewji amewasihi mashabiki wa timu hiyo kutofadhaishwa na matokeo na kiwango cha timu kwa mechi mbili zilizopita na kuendelea kuisapoti timu.

“Nawaomba tusitoke kwenye reli. Tupambane. Nguvu Moja,” aliandika Dewji katika ukurasa wake wa Instagram.

Kauli hiyo ya Dewji imeungwa mkono na nyota wa zamani wa timu hiyo ambao sasa ni makocha, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na Ulimboka Mwakingwe ambao wameshangazwa na tuhuma zinazoelekezwa kwa benchi la ufundi wakidai hazina mashiko.

“Simba hawajaanza vibaya sana, pia hawajaanza vizuri lakini ninachokiona, bado timu na wachezaji hawajawa katika ule ubora uliozoeleka kama ilivyokuwa msimu uliopita, sasa ndio inaonekana kama wanazidiwa au hawapati kile kinachotegemewa lakini nakuhakikishia kama ndani ya muda mfupi watarudi katika kiwango kile cha nyuma, basi hakuna atakayeigusa.

Suala la mfumo au kucheza ugenini mimi sioni kama ni sababu kwa kuwa hata msimu uliopita timu ilipata mafanikio kwa kutumia mfumo huo, pia ilipata ushindi wa mabao mengi hata katika viwanja vya ugenini.

Bado Simba haijafikia asilimia 100 za ubora wake. Achana na kiwango walichokionyesha katika mechi ya Simba Day au ile ya Ngao. Naamini watakaa sawa na mashabiki watafurahi. Uzuri mashabiki wengi wa Simba ninavyowafahamu, wanajua na wanauelewa vilivyo mpira wa miguu hivyo wanapoona jambo fulani haliko sawa hawasiti kujionyesha kuwa hawajafurahi,” alisema Mwakingwe.

Kwa upande wake Julio alisema mashabiki na wote wanaomlaumu Vandenbroeck wanapaswa kujitafakari.

“Mwalimu anapokuja anakuwa na falsafa yake. Mimi nikiwa kocha nikasema nataka hiki basi inatakiwa kitimizwe na sio watu wanipangie wanachokitaka.

Kocha kwa utashi wake anaona mfumo wa kucheza na straika mmoja ndio unamfaa hivyo watu wanapaswa kumheshimu na sio kuanza kumwingilia kwa sababu hicho ndicho alichojifunza na anachokiamini.

Kama wanaona hayuko sawa, wangoje aondoke halafu akija mwingine ndio kifanyike hicho wanachokitaka,” alisema Julio.

Mbali na Mwakingwe na Julio, nyota wa zamani wa Pamba, Hamisi Ramadhan ambaye ni baba wa beki Hassan Kessy wa Mtibwa naye ameonyesha kumtetea Vandenbroeck

“Kocha ana mfumo wake anaoutumia. Sasa hivi ameona ule wa kutumia straika mmoja ndio unaomfaa muda huu kwa sababu Bocco (John) anafanya vizuri.

Naamini Bocco asipofanya vizuri mechi zijazo, Kagere atacheza, pia hata kutumia washambuliaji wawili huko siku za mbeleni kwa sababu mechi ziko nyingi na ligi ni ngumu.

Jambo kama hilo ndilo liliwagharimu Mtibwa Sugar katika mechi nyingi msimu uliopita lakini kwa sasa kocha wao kabadili mfumo na wanaonekana wako vizuri sio kama ilivyokuwa nyuma,” alisema Mzee Hamisi Ramadhan.

Katika mechi mbili za kwanza za Ligi Kuu, Simba ilianza kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Ihefu huko Mbeya na mechi iliyofuata walitoka sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar.