MAONI: Dila la Samatta liwaamshe wengine

Monday January 20 2020

 

DILI tayari limeshatiki kwa Straika na Nahodha wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta kutua kwenye Ligi Kuu England kuitumikia Klabu ya Aston Villa.

Kitendo hicho kilikuwa ni ndoto ya muda mrefu ya Samatta na sasa kimeonekana kutimia. Kinachosubiriwa ni Aston Villa kutangaza uhamisho huo unaomuondoa staa huyo kutoka KR Genk ya Ubelgiji.

Tangu alipoondoka Tanzania mwaka 2011 alipokuwa akiitumikia Simba Sport Club na kujiunga na TP Mazembe, Samatta ameonyesha uwezo, kiu na nia ya kuyatafuta mafanikio.

Tofauti kabisa na wachezaji wengine waliowahi kutoka nje kabla yake, Samatta aliongeza juhudi na maarifa binafsi na hakuuendekeza U-supastaa aliokuwa nao, bali alijituma na kufanya kila jitihada kuhakikisha anafika pale anapotoka, leo hii anakuwa mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kucheza Ligi Kuu England (EPL).

Sio kama Samatta hakukumbwa na mitihani na vishawishi vya kuzuia ndoto zake za kutua katika mojawapo mwa ligi kubwa duniani, lakini nyota huyo wa Tanzania alijitahidi kadiri alivyoweza kuvishinda vishawishi na mitihani ili kuweza kutimiza malengo yake makuu.

Mwanaspoti tunafahamu inahitajika jitihada kuweza kufikia malengo kama ya Samatta lakini hakuna budi pale mtu anapodhamiria kutimiza lake.

Advertisement

Kwa kuyatambua hayo, ndio maana leo tunarudi kwa vijana wa Kitanzania ambao wana ndoto za kutaka kucheza Ligi Kuu za England (EPL), ya Ujerumani (Bundesliga), Hispania (La Liga), Italia ( Seria A) na Ufaransa (League 1) na kuwataka kufanya jitihada za ziada.

Hivi sasa Samatta amekuwa kama dira ya kila kijana wa Kitanzania anayetaka kucheza soka la mafanikio nje ya nchi.

Tunawaambia vijana wa Kitanzania ni rahisi sana kusema wanatamani kufuata nyayo na kuwa kama Samatta lakini inahitajika kazi, uvumilivu na jitahada kufikia ndoto hizo.

Mwanaspoti halina lengo la kuwakatisha tamaa na kuamini hakuna Mtanzania mwingine anayeweza kutimiza ndoto hizo, la hasha. Hata Samatta mwenyewe anaamini wapo vijana wanaoweza kupita njia zake na kupata mafanikio tena zaidi yake.

Ndio maana mara kwa mara, Samatta amekuwa akiwatia moyo wachezaji wengine kufanya maandalizi mazuri ili wapate mafanikio kama yake na kuliwezesha taifa kuwa na mafanikio makubwa.

Samatta na Watanzania kwa ujumla wetu tunaamini kama tutakuwa na wachezaji wengi katika nchi za Ulaya na baadhi za Afrika tunaweza kufanya vizuri kimataifa.

Kama hilo likitimia tutakuwa na wachezaji wanaojitambua kwa kujitunza vizuri, kujua miiko yao na hata kutoa ushindani kwa mataifa mengine.

Mbali hivyo, pia wachezaji hao wanaweza kulitanga zaidi taifa letu nje ya nchi kwa kuwaeleza vivutio vinavyopatikana nchini na kukuza utalii kama anavyofanya Samatta.

Kwa kufanya hivyo, taifa litakua kiuchumi na kuongeza kipato katika hazina yetu. Hivyo mbali na wachezaji kuwa na maisha mazuri lakini pia walitaliwezesha taifa kuwa na uchumi imara kwa kuwa watakuwa mabalozi wetu huko wanakokwenda.

Ndio maana tunasema wengine nao wafuate nyao, maana Samatta ameonyesha inawezekana. #Hainakufeli.

Advertisement