Liuzio: Kwa usajili wa Kalengo Yanga imelamba dume

Monday July 15 2019

 

By Mwanahiba Richard

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Juma Liuzio amewaambia Yanga wanahitaji kuvumilia kidogo nyota wao mpya Maybin Kalengo kutokana na umri wake lakini mguuni ana madini ya kutosha.

Liuzio aliyewahi kuichezea Zesco ya Zambia aliyotokea Kalengo ameliambia Mwanaspoti kuwa katika sajili bora ambazo Yanga wamezifanya msimu huu basi moja wapo ni usajili wa Kalengo.

Liuzio alisema anamfahamu mchezaji huyo kwani walikuwa wote Zesco ingawa Kalengo alipandisha kutoka timu yao ya vijana.

"Unaweza kumwangalia mchezaji ukaona kabisa kuwa huyu atashindwa kwa mpira wa Tanzania ama mfumo wa timu fulani, lakini sio kwa Kalengo. Kama Yanga watamtumia vizuri basi watanufaika naye.

"Ni mchezaji mzuri, ila wamvumilie maana umri wake bado mdogo alipandishwa kutoka timu ya vijana, ana nguvu hivyo kwa mpira wa Tanzania ataweza kucheza. Pia hata nafasi ndani ya Yanga ana uwezo wa kupenya kikosi cha kwanza endapo tu mwalimu wake ataona inafaa.

"Wakati Yanga wanamuhitaji aliniuliza juu ya timu hiyo na mazingira halisi ya soka letu kwamba kitu gani kinahitaji ili atakapokuja ajue anakuja kufanya nini, nilimsaidia kumwelekeza baadhi ya mambo na maisha ya mpira wetu hivyo naamini ataweza," alisema Liuzio.

Advertisement

 

Advertisement