Kumbe tatizo Prisons ni ushambuliaji

Nahodha wa Tanzania Prisons, Laurian Mpalile

Muktasari:

Laurian Mpalile ambaye ni nahodha wa Prison amesema, msimu ulioisha walimaliza katika nafasi nzuri za tano bora katika msimamo lakini kwa sasa upepo umewaendea vibaya msimu huu kutokana na kushindwa kupata matokeo mazuri katika michezo tuliyocheza.

NAHODHA wa Tanzania Prisons, Laurian Mpalile amemuomba kocha wa timu hiyo kuhakikisha anafanyia kazi eneo la ushambuliaji katika usajili wa dirisha dogo kwa kuwa chipukizi wameshindwa kwenda na kasi ya Ligi Kuu Bara msimu huu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mpalile alisema msimu huu kikosi chao kimepitiwa na upepo mbaya uliosababisha kushindwa kuanza vizuri na kujikuta wakiwa katika nafasi mbaya katika msimamo wa ligi.

Alisema kabla ya msimu haujaanza, kikosi chao kilitoa baadhi ya wachezaji ambao mikataba yao iliisha na baadaye uongozi haukuangaika kusajili na kujikuta ukipandisha nyota wengi kutoka kikosi B kitu ambacho kinatakiwa kutoa muda zaidi kwa wachezaji hao ili wazoee ligi.

“Timu yetu sio mbovu sana kama inavyochukuliwa, tuna timu nzuri lakini kinachotuangusha ni kujaza chipukizi wengi ambao hawana uzoefu katika eneo la ushambuliaji ambalo ni muhimu. Tuna vijana wengi kutoka timu B jambo ambalo limekuwa likitukosesha matokeo,” alisema.

“Mwalimu anatakiwa kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji kwa kusajili mchezaji mwenye uzoefu, ambaye ataweza kuwapa changamoto nyota wanaochipukia najua soka la saizi linachezwa na vijana, lakini sio muda wake kuendelea kuwapa nafasi zaidi timu ikiwa katika nafasi mbaya,” alisema.

Mpalile aliongeza kuwa wanatarajia kuona Prisons ya mabadiliko zaidi mara baada ya dirisha dogo la usajili kupita na kuondokana na changamoto ya kushindwa kupata matokeo katika kila mchezo wanaoucheza kitendo ambacho kinawaumiza wao kama wachezaji.

Alisema hawana tatizo lolote na wapo vizuri na mwalimu kinachowaangusha ni kuwa na kikosi kilichojaa nyota wengi waliokosa uzoefu na kuongeza kuwa wanaamini baada ya muda wataweza kuwa sawa na kuirudisha Prisons katika ushindani.