Koeman ajitoa sakata la Messi kuondoka

Barcelona, Hispania. Kocha wa Barcelona, Ronald Koeman amesema hana tatizo na nahodha wa timu hiyo Lionel Messi kutokana na sakata zima la nyota huyo kutaka kuondoka na baadaye kuamua kubaki.

Mshambuliaji huyo wa kiamatifa wa Argentina aliiambia Barcelona kwa ujumbe wa fax, kuwa anataka kuondoka Nou Camp msimu huu, lakini alibadili uamuzi huo na kutangaza kuwa atabaki kwa msimu mmoja zaidi.

Koeman, ambaye aliajiriwa kama kocha Agosti baada ya kutimuliwa kwa Quique Setien, alibainisha kuwa hakuhusika kwa namna yoyote na sakata la mzozo wa Messi na klabu.

“Hilo lilikuwa tatizo lao, halinihusu hata kidogo,” alisema Koeman alipozungumza na mtandao wa Fox Sports.

“Hiyo ilikuwa ni kati ya Messi na klabu. Nilizungumza na Messi tangu wakati huo na kukubaliana kuwa tutaendelea kufanya kazi pamoja.”

Nyota huyo wa miaka 33 alihusishwa na kutua Manchester City ya Ligi Kuu England baada ya kuomba kuondoka.

Badala yake, alithibitosha kuwa atabaki Barcelona hadi mwisho wa msimu wa 2020/21, kwasababu klabu ilifunga vipengele vya usajili wake.

“Nitaendelea kubaki katika klabu hii kwasababu rais ameniambia njia pekee kwa mimi kuondoka ni kwa mimi kulipa kiasi cha Pauni 625 milioni, hilo haliwezekani,” alisema Messi.