Kocha Mayanja hatihati KMC

Muktasari:

Mayanja alianza kukosekana kwenye benchi la timu hiyo Jumatatu ya wiki hii wakati KMC ikiilaza Biashara United mabao 2-1 mchezo uliopigwa Uwanja wa Uhuru, huku taarifa za awali zilieleza kocha huyo amepata udhuru.

HUKO KMC sasa mambo yanaelekea kufikia mwisho kwa Kocha Jackson Mayanja ambaye alianza kazi ya kukinoa kikosi hicho mwezi Juni akichukua mikoba ya Etienne Ndayiragije.

Chanzo cha kuaminika kimelidokeza Mwanaspoti jana Ijumaa kwamba kocha huyo raia wa Uganda ameuandikia uongozi wa timu barua ya kuvunja mkataba kutokana na sintofahamu inayoendelea kwa upande wake.

“Kocha bado haendelei na kazi kutokana na kukosa vibali na hajatafutiwa mpaka sasa, na leo (jana) hatakuwepo pia kwenye mchezo huo kwa maana suala lake bado halijapatiwa ufumbuzi na sidhani kama kutakuwa na lolote jipya kwa hivi karibuni,” kilieleza chanzo hizo.

Mayanja alianza kukosekana kwenye benchi la timu hiyo Jumatatu ya wiki hii wakati KMC ikiilaza Biashara United mabao 2-1 mchezo uliopigwa Uwanja wa Uhuru, huku taarifa za awali zilieleza kocha huyo amepata udhuru.

Baadaye Mwanaspoti liligundua alikosekana kwa sababu ya kuitwa na Idara ya Uhamiaji kutokana na kufanya kazi nchini bila kuwa na vibali, na hata alipotafutwa aliliambia Mwanaspoti uongozi unajua kila kitu juu yake.

Katibu msaidizi wa KMC, Walter Harrison alipoulizwa kama kocha huyo angeweza kuwepo kwenye mchezo wa jana Ijumaa alisema, “kwa sasa tupo kwenye pilika ya mchezo mengine tutaongea baada ya mchezo kumalizika.”

Wakati suala la Mayanja likiendelea kutafutiwa ufumbuzi na uongozi wa timu hiyo, kocha msaidizi Mlage Kabange alisema wala hana presha kutekeleza majukumu yake wakati bosi wake akiwa pembeni kwa muda usiojulikana.

“Tunashukuru Mungu hali ya kikosi ipo vizuri na (timu) inaendelea na programu ikiwa chini yangu, kwa sababu vitu ambavyo tunapaswa kuvifanya ni vilevile vitu vinavyofaywa kila siku, ndivyo ninavyovifanya na kunisaidia kupata matokeo mchezo wa Biashara,” alisema Kabange.

Mwenyekiti wa timu hiyo, Benjamin Sitta siku mbili zilizopita alisema suala la Mayanja linafanyiwa kazi na pia unatazamwa uwajibikaji (perfomace) ya timu ndio inayoweza kumbakiza au kumuondoa kocha huyo kuendelea kuinoa timu. KMC ilipanda daraja msimu wa 2018/19 ikiwa chini ya kocha fred Felix Minziro ambaye baadaye aliondoka na mikoba yake kuchukuliwa na Ndayiragije.