Mayanja ajivunia kurudi kwa nyota wake KMC

Muktasari:

KMC inaendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo wa Ligi dhidi ya JKT Tanzania mchezo unaotarajiwa kuchezwa Oktoba 19 mwaka huu.

Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa KMC, Jakson Mayanja amesema anatarajia kuanza kuumiza kichwa kusuka upya kikosi cha ushindani baada ya wachezaji wake wengi waliokuwa majeruhi kupona.

KMC imecheza michezo minne na kuambulia pointi nne baada ya kushinda mchezo mmoja sare moja na kukubali kipigo cha michezo miwili.

Wachezaji majeruhi wa KMC ni pamoja na mshambuliaji Charles Ilanfya, kiungo Cliff Buyoya, beki Yusuph Ndikumana na Salum Aiyee sasa amerudi katika hali ya kawaida baada ya daktari wa timu hiyo kukubali wanaweza kuanza kucheza.

Mayanja alisema wanatarajia kuanza na JKT Tanzania mara baada ya kupisha mchezo wa kirafiki kwa timu za Taifa hivyo huo utakuwa ni mchezo wake muhimu kusuka kikosi cha ushindani.

Alisema ni anaimani na wachezaji wake waliorudi kikosini na anategemea kuona changamoto ya ushindani kutoka kwa wachezaji ambao wanacheza nafasi moja ili kila mmoja aweze kumshawishi kumpa namba katika kikosi cha kwanza.

"KMC ilifanya usajili mzuri changamoto ilikuwa ni wachezaji wengi walipata majeruhi katika michezo ya kirafiki ikiwa ni sambamba na nafasi tuliyopata ya kushiriki mashindano ya kimataifa kwa Kombe la Shirikisho," alisema Mayanja.