Kisinda, Junior waipaisha Yanga

Muktasari:

Huo ni ushindi wa pili mfululizo kwa Kocha Kaze tangu apewe majukumu ya kuiongoza timu hiyo akichukua mikoba ya Zlatiko Krmpotic.

Mwanza. Mabadiliko aliyoyafanya Kocha Mkuu wa Yanga, Cedrick Kaze kumtoa Deus Kaseke na kumwingiza Farid Mussa yameonekana kuzaa matunda kwa timu hiyo.

 

Kaze alifanya mabadiliko hayo dakika ya 57 ambapo Farid akitokea benchi aliweza kupiga kona iliyozaa bao la pili dakika ya 61 kupitia kwa Wazir Junior.

 

Kuingia kwa bao hilo kuliiamsha Yanga ambao walionekana kushambulia sana na kuwapa wakati mgumu wapinzani wake KMC.

 

Hata hivyo kabla ya kupatikana kwa bao hilo, Lamine Morro na Sarpong walijikuta wakioneshwa kadi za njano kwa muda tofauti kutokana na kuwacheza rafu wapinzani wao.

 

Pia KMC nao chini ya Kocha wao, Habibu Kondo alifanya mabadiliko ya kuwatoa Kabunda, Abdul Hilary na Gean Muigiraneza kuwaingiza Reliant Lusajo na Martin Kigy na Cliff Buyoya.

 

Pia Kaze hakuishia hapo na kuwatoa Junior na Kisinda na kuwaingiza Haruna Niyonzima na Abdalah Shaibu, mabadiliko ambayo yaliiwezesha Yanga kuondoka na alama tatu muhimu na kufikisha alama 19, huku KMC wakibaki na alama zao 13 baada ya mechi saba kwa pande zote.

 

Bao la kwanza liliwekwa wavuni na Tuisla Kisinda kwa mkwaju wa penalty dakika ya 41 baada ya mshambuliaji Michael Sarpong kuchezewa madhambi ndani ya boksi na la KMC lilifungwa kwa shuti kali nje ya boksi lililopigwa na Hassan Kabunda dakika ya 27.