Kisa jezi: Usimba, Uyanga waibuka mechi za vijana Uganda, Angola

Monday April 15 2019

 

By Doris Maliyaga na Thomas Ng'itu

Dar es Salaam. Usimba na Uyanga umeibuka katika mchezo wa pili ya fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17, kati ya Uganda na Angola.

Iko hivi, katika mchezo huo ulioanza kutimua vumbi majira ya saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Angola iliingia ikiwa wamevaa tisheti za jezi za rangi nyekundu na bukta nyeusi zikiwa na ufito mweupe pembeni na kufanya rangi nyekundu kuonekana kwa wingi.

Uganda ambayo ni majirani wa Tanzania na wanatoka ukanda wa Afrika Mashariki,  wamevaa tisheti za njano na bukta zenye rangi nyeupe na ufito mwekundu pembeni na kufanya rangi ya njano ionekane kwa wingi.

Hali hiyo imewafanya sehemu kubwa ya mashabiki wanaopenda kukaa upande wa Simba kuishangilia Angola.

Hii ni kwa sababu Simba wao huwa wanatumia jezi za rangi nyekundu kucheza mechi zao wanapokuwa nyumba, wakati watani wao Yanga hutumia njano.

Advertisement

Shabiki mmoja aliyekuwa upande wa jukwaa ambalo mara nyingi hutumiwa na mashabiki wa Simba alisikika akisema, piga Uganda hao, jezi zao zina gundu (akimaanisha mkosi) kwa sababu watani wao Yanga ndiyo wanavaa.

Hata hivyo, mbali na rangi ya jezi hizo, sehemu kubwa ya Watanzania walitarajiwa kuiunga mkono Uganda ambao ni majirani.

Katika mchezo huo Angola ilibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Uganda.

Katika mchezo huo ulikuwa wa pili katika ufunguzi wa Fainali za Afcon nchini, Angola walipata goli la mapema dakika 33 kupitia kwa winga Osvaldo Pedro.

Kipindi cha kwanza cha mchezo huo Angola walikuwa wakitawala mpira baada ya kutumia njia ya kupiga mipira mirefu kiasi ambacho kilikuwa kikiwatesa Uganda katika kuzuia njia hiyo.

Hata hivyo walipotoka kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wachezaji wa Uganda walionekana kubadilika na kuanza kucheza mchezo wa kushambulia zaidi tofauti na kipindi cha kwanza.

Mawinga wawili wa Angola, Pedro aliyefunga bao na Zito Luvumbo walikuwa wakiisumbua mno ngome ya Uganda hata hivyo mabeki wa Uganda walionyesha umakini katika kuzuia.

Uganda nao walikuwa wakijibu mapigo na walifika mara kadhaa katika lango la Angola na kupiga mashuti ambayo kipa wao Geovani Carvalho alionyesha umahiri wa upangua michomo hiyo.

Advertisement