Kipa Taifa Stars shangwe tupu kupenya Afcon

Muktasari:

 Wachezaji 23 watakaowakilisha Tanzania katika mashindano hayo wameshajulikana baada ya kutemwa wachezaji 16 waliokuwepo katika kikosi cha awali. 

Dodoma. Baada ya kikosi cha timu ya Tanzania (Taifa Stars) kuwekwa wazi kwa wachezaji 23 watakaocheza fainali za mataifa ya Afrika (Afcon), kipa wa timu hiyo Aaron Kalambo amesema kwake ni rekodi.

Kalambo anayeichezea Tanzania Prisons, alisema kuwepo katika kikosi hicho kwake ni zaidi ya furaha kwani atabaki katika historia ya wachezaji waliocheza mashindano hayo.

"Nimefurahi mno kuwa katika wachezaji 23 watakaowakilisha nchi katika fainali za mwaka huu nchini hapa na kwangu ni zaidi ya historia," alisema Kalambo.

Kalambo amekiri kupata ofa kutoka kwa timu kubwa  zinazomhitaji, aliongeza kuwa endapo atapata nafasi ya kucheza katika mchezo wowote itakuwa ni zawadi kwa familia wazazi wake na familia kwa ujumla waliopo wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.

"Najiamini nina ubora stahiki ndio maana benchi la ufundi limenijumuisha katika kikosi cha mwisho hivyo natarajia pia nikipangwa mchezo wowote nitafanya makubwa na itakuwa zawadi kwa wazazi wangu na ndugu zangu kwa ujumla."

Kuhusu nafasi ya Taifa Stars katika Kundi C ikiwa pamoja na timu za Senegal, Kenya na Algeria, Kalambo alisema wao kama wachezaji watapambana kupata matokeo chanya.

"Kwa ujumla wachezaji wote tuna morali ya juu ambayo inatufanya tuamini tutafanya vizuri na kuwaziba mdomo wanaodhani hatuwezi,"alisema Kalambo.

Taifa Stars inatarajiwa kucheza mchezo wa kwanza wa kirafiki kesho Alhamisi dhidi ya Misri kwenye Uwanja wa jeshi, Borg el Arab uliopo mjini Alexandria nchini Misri.