Kipa Mtanzania ainusuru Gor Mahia na kipigo cha Moteme Pembe

Monday October 28 2019

 

By THOMAS NG'ITU

Dar es Salaam.Kipa Mtanzania David Kisu Mapigano ameibuka shujaa baada ya kuokoa penalti na kuisaidia timu yake Gor Mahia kupata sare 1-1 dhidi ya DC Motema Pembe katika mchezo wa kwanza Kombe la Shirikisho Afrika.

Mapigano aliokoa penalti hiyo iliyopigwa na Vinny Bogonga wa Motema Pembe katika dakika za mwisho za kipindi cha pili na kufanya mchezo huo kumalizika kwa sare 1-1 kwenye Uwanja wa Kasarani.

Gor Mahia ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Gnamien Yikpe kabla ya DC Motema Pembe kusawazisha kupitia kwa William Luenzi.

Uwezo wa kipa Mapigano unazidi kuimarika ndani ya kikosi cha Gor Mahia tangu alipojiunga nayo akitokea Singida United msimu huu.

Katika mchezo huo kipa Mapigano mbali ya kuokoa penalti hiyo alifanya kazi kubwa kuzuia washambuliaji wa DC Motema Pembe wasipate bao.

Beki wa Gor Mahia, Charles Momanyi alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kushika mpira uliokuwa unaingia golini na kusababisha penalti. Mshambuliaji wa Motema Pembe, Vinny Bangonga Kombe alipiga penalti hiyo na kuokolewa na kipa Mapigano.

Advertisement

Wakati matokeo yakiwa 1-1, Motema Pembe ilifanya shambulizi la kushtukiza kupitia Misoko Amale aliyepiga krosi safi kutokea upande wa kulia na kumkuta Junior Mbele akiwa peke yake ambaye alipiga kichwa kilichookolewa na Mapigano uliporudi kwa mshambuliaji huyo alipiga shuti ndipo Momanyi alipoushika mpira huo.

William Likuta Luezi alifunga bao la kusawazisha la Motema Pembe, akifuta lile lililofungwa mapema na Gnamin Yikpe mwanzoni mwa kipindi cha pili. Luezi alikuwa mwepesi kuwahi mpira uliokolewa na kipa Mapigano aliyefanya kazi nzuri kuokoa mpira uliopigwa na Junior Kone Abou.

Mapema Mapigano alifanya kazi nzuri kuokoa hatari mbili za mshambualiji Herritier Ngouelou aliyekuwa katika kiwango cha juu katika mchezo huo.

Advertisement