Kinara wa mabao ASFC afunguka

Muktasari:
Yassin licha ya timu yake kuishia hatua ya 16 bora baada ya kutolewa na Sahare All Stars ya FDL amesema kwa upande wao ni mafanikio makubwa kuiwezesha timu hiyo kuwa kwenye orodha ya timu 16 kwenye ASFC.
MFUNGAJI Bora wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), Omary Yassin ameeleza mafanikio aliyoyapata msimu uliomalizika akiwa na timu yake ya Panama FC kuwa ni kujitoa zaidi kwa wachezaji wa timu hiyo.
Yassin licha ya timu yake kuishia hatua ya 16 bora baada ya kutolewa na Sahare All Stars ya FDL amesema kwa upande wao ni mafanikio makubwa kuiwezesha timu hiyo kuwa kwenye orodha ya timu 16 kwenye ASFC.
Akizungumza na Mwanaspoti Online leo umatatu Agosti 3, 2020, Yassin amesema: "Nimemaliza nikiwa kinara wa mabao tisa niliyofunga katika michezo minne niliyocheza na baadaye kupata majeraha, imekuwa heshima kubwa kwangu na timu yangu.
"Kuchukua tuzo nimejisikia furaha japo lengo letu ilikuwa kufika fainali na msimu ujao tutajitahidi tupite pale tulipoishia ili ikiwezekana tuvae medali," amesema Yassin
Amesema msimu ujao watajitahidi kufanya vizuri zaidi na ikiwezekana hata kufika fainali na kuwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa.
Yassin alifunga mabao yake katika mchezo dhidi ya Magereza FC akipiga hat-trick walipoibuka na ushindi wa mbao 4-1, akatupia nne kwenye ushindi wa mabao 6-4 mbele ya Timberland FC na akafunga bao moja moja dhidi ya Eagles FC na Area C walipoichapa 2-1.
Baada ya mchezo dhidi ya Area C kinara huyo hakuonekana uwanjani kutokana na kuumia goti lililomweka nje kwa muda mrefu.